Wilaya ya Chato, mkoani Geita, imeiomba serikali kupitia mamlaka husika kuongeza idadi ya majiko ya gesi ya ruzuku kutokana na ongezeko kubwa la wananchi wanaojitokeza kupata majiko hayo. Mpango huu unalenga kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, na hivyo kuhamasisha matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa majiko hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Chato, Thomas Dimme, alisema wilaya hiyo imepatiwa jumla ya majiko 3,255. Hata hivyo, alibainisha kuwa idadi hiyo haitoshelezi mahitaji ya wananchi, ambao wameonyesha mwamko mkubwa wa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi.



Majiko haya ya gesi yametolewa kupitia fedha za ruzuku, huku kila kaya ikitakiwa kuchangia shilingi 17,500. Akifafanua kuhusu mpango huo, Mhandisi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Frances Manyama, alisema kaya zinazostahili kupata majiko hayo zinapaswa kufika na kitambulisho cha NIDA. Hii inalenga kuhakikisha ugawaji unafanyika kwa uwazi na kila kaya inapata jiko moja pekee.



Wananchi waliopokea majiko hayo wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema kuwa utasaidia kupunguza ukataji miti na hivyo kutunza mazingira. Mzee Boniface Mnaku, mmoja wa wanufaika, alisema, “Tunashukuru serikali kwa mpango huu. Majiko haya yatapunguza gharama za nishati na kulinda mazingira yetu dhidi ya ukataji ovyo wa miti.”



Wananchi wa Wilaya ya Chato sasa wanasubiri kwa hamu hatua za serikali katika kuongeza idadi ya majiko ya gesi ili kukidhi mahitaji yao makubwa.




Share To:

JOEL MADUKA

Post A Comment: