Na Denis Chambi, Tanga.
MAMLAKA ya Maji bonde la mto Pangani inayosimamia mikoa ya Tanga Kilimanjaro Arusha na baadhi ya sehemu za Mkoa wa Manyara imesema kuwa itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wananchi ambao wamekuwa wakitumia huduma ya maji bila ya kuwepo na vibali maalum hali ambayo imekuwa ikichangia uharibufu wa miundombinu.
Akizungumza katika kikao cha tatu cha jukwaa la wadau wa usimamizi wa rasilimali za maji katika kidakio cha mto Umba kilihofanyika wilayani Lushoto Mkurugenzi wa bonde la mto Pangani Segule Segule amesema kuwa watu wawili wamefikishwa mahakamani baada ya kukutwa na kosa hilo ambapo amewataka wananchi kuendelea kuhimizana kuimarisha ulinzi baina yao ikiwa ni takwa la kisheria.
"Sisi tutaendelea kusimamia na kuchukua hatua stahiki kwa kulingana na mazingira wasiolipa tunao kanzi data yetu na tunawafwatilia jitihada zinaendelea kufanyika tunaamini viongozi waliopo hawatovumilia hilo lakini wale ambao watakaidi sheria iko wazi na ikibainika kwamba kuna aliyekaidi sheria imeelekeza pia afungwe jela" amesema Segule
"Bonde tunaendelea kuwahimiza wananchi kuwa tusipoheshimu taratibu zilizowekwa tutapata madhara jamii nzima kwahiyo tuhimizane tuishi kwenye jukumu la kuvitunza vyanzo vyetu vya maji hii itatutupelekea kutunusuru sisi sote kuanzia ngazi za mtu binafsi familiya na jamii kwa ujumla"
Ameongeza kuwa Mkoa wa Tanga una jumla ya vyanzo vya maji 544 lakini ni vyanzo 40 pekee vilivyowekewa alama za utambuzi ili kivinusuru na uharibufu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu huku mamlaka ikiendelea na hatua mbalimbali ya kuvilinda pamoja na kuibua vyanzo vingine vipya ili kuwa na uhakika wa maji safi na salama wakati wote.
"Tanga vipo vyanzo vya maji 544 tukivyoviainisha kati ya hivyo ni takribani 40 ndivyo vilivyowekewa alama za mipaka tunategemea Kwa kushirikiana Kwa pamoja na viongozi wa ngazi za chini vyanzo vyote vilivyopo vitawekewa mipaka na baadhi ya vyanzo vipya tutavitambua"
Akifungua kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Korogwe William Mwakilema amezitaka Jumuiya za watumia maji zilizopo katika jamii kutimiza takwa la kisheria kulipia na kuomba vibali na kulipia ada za matumizi ya maji bila kushurutishwa.
"Nitoe rai kwa wadau wanaotumia huduma ya maji kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha mpango kazi wa utunzaji wa vyanzo vya maji katika maeneo yetu unakuwa endelevu zipo jumuia za watumia maji ambazo hamjaomba na kulipa ada za matumizi ya maji kwa bonde kama sheria inavyoelekeza"
Shadrack Mwambene Afisa tarafa wa kata ya Umba wilayani Lushoto ameeleza changamoto ambayo wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakikabiliana nayo kwa muda mrefu ambapo wamekuwa wakitumia maji machafu hali ambayo unaweza kuleta athari kwa jamii .
"Katika maeneo ya kwetu wapo baadhi ya wananchi wanatumia maji Bure kabisa bila ya kusimamia na RUWASA wala watu wa bonde lakini Kuna maji tunayotumia ambayo ni machafu hayajawekewa kinga yeyote Mimi na familiya yangu ni wahanga wa magojwa ya tumbo kutokana na kutumia maji machafu" amesema Mwambene.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya watumia maji katika mto Mbaramo Zakayo Ngiyoko ameahidi kuwa balozi wa kusimamia na kutekeleza takwa la kisheria la kuendelea kuwahimiza wananchi waliopo katika jumuia za watumia maji kuwa walinzi na wasimamizi wa rasilimali za maji zilizopo katika maeneo yao.
"Kwa kupitia kikao hiki ambacho tumepewa miongozo na maelekezo mbalimbali tumefarijika na tunakwenda kutekeleza na kusimamia rasilimali za maji kwa uzuri" amesema Ngiyoko.
Post A Comment: