Bodi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imekamilisha ziara ya siku tatu katika mikoa ya Dodoma na Manyara, ikilenga kukagua utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na maendeleo ya utalii wa ikolojia.
Ziara hiyo ilianza Wilaya ya Kondoa, ambako bodi ilitembelea maeneo ya michoro ya watu wa kale, urithi wa kihistoria wenye mchango mkubwa katika kuvutia watalii na kuhifadhi utamaduni wa kale. Baadaye, wajumbe wa bodi walitembelea Milima ya Hanang’, ambapo walikagua athari za utalii wa ikolojia katika uhifadhi wa misitu ya asili na ustawi wa jamii zinazozunguka eneo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara, mjumbe wa bodi, Dkt. Siima Bakengesa, alieleza kuridhishwa na juhudi za TFS katika kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii wa ikolojia. “Tumeona juhudi kubwa za TFS katika kuongeza idadi ya watalii na mapato kupitia utalii wa ikolojia. Eneo la Hanang’ ni mfano wa mafanikio ya ulipiaji wa huduma za mfumo wa ikolojia, ambao unasaidia kuongeza kipato kwa wakulima na kuimarisha uhifadhi wa misitu,” alisema.
Dkt. Bakengesa pia alitoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo yanayohifadhiwa na TFS ili kuchochea ukuaji wa utalii wa ikolojia na kufanikisha lengo la kufikia watalii milioni tano. Alisisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Aidha, alibainisha kuwa TFS imechukua hatua madhubuti kuboresha huduma za watalii kwa kujenga njia maalum na ofisi za kupokea wageni, hatua zinazolenga kuongeza ubora wa huduma na kuvutia wageni wengi zaidi.
Ziara hiyo imebainisha juhudi za TFS katika kuhifadhi rasilimali za misitu na kukuza utalii wa ikolojia, ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya taifa na kuboresha maisha ya jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa.
Bodi hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na TFS katika kufanikisha malengo ya uhifadhi na maendeleo ya utalii endelevu.
Post A Comment: