📌 Dkt. Biteko asema nia njema ya Rais Samia iungwe mkono kuleta maendeleo kwa Watanzania
📌 Ampongeza Mbunge Kiswaga kwa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo Wilaya ya Magu.
Amesema hayo leo Desemba 23, 2024 wilayani Magu mkoani Mwanza katika Mkutano Mkuu Maalum ambapo taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa mwaka 2020 hadi 2024 iliwasilishwa.
“Mhe. Rais amefanya kazi kubwa ya kupigiwa mfano na anastahili pongezi, nataka niwaambieni kuna watu wengine wanaumia tukimpongeza Rais Samia, lakini wajue hatutoi pongezi hizi peke yetu hata huko duniani kwa mfano Benki ya Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanampongeza kwa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa asilimia 5.1,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema pia kuwa Rais Samia ana nia njema na anataka kuona Watanzania wanapata maendeleo.
Ameongeza kuwa maendeleo katika Jimbo la Magu hayakuja kwa bahati mbaya isipokuwa kwa mipango na hivyo anawapongeza wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Magu kwa tamko la pongezi kwa Rais Samia kwa kuwapa fedha kiasi cha shilingi 143.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa na Serikali “ Barabara za lami zimeunganisha mikoa yote nchi nzima, tuna ndege za abiria na mizigo, tumejenga shule nyingi na sasa tunajenga shule za kata maeneo mbalimbali nchini. Maendeleo yanaonekana kwa macho na sisi ni kazi yetu kusema haya kwa wivu mkubwa,”
Kuhusu umeme Dkt. Biteko amesema katika kijiji kimoja pekee ambacho hakina umeme, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya kupeleka umeme huku mipango ya kupeleka umeme katika kisiwa ikiendelea.
Aidha, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Magu, Mhe. Kiswaga kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Dkt. Biteko amesema “CCM ni chama kiongozi hivyo wanaCCM tembeeni kifua mbele hubirini yanayofanywa na chama chenu waonesheni watu maendeleo yaliyotokea msiwapuuze,”
Pamoja na hayo amempongeza Mhe. Kiswaga kwa kusimamia miradi ya maendeleo huku akiwaasa wanachama wa CCM kushirikiana na viongozi kwa ngazi zote ili kuendelea kuimarisha chama huku akiwapongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Jimbo lao.
Mbunge wa Jimbo la Magu, Mhe. Boniventura Kiswaga wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu Jimbo la Magu kwa mwaka 2020 hadi 2024 amesema Serikali ya Rais Samia imeendelea kuwapa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo shilingi bilioni 78 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wametoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kujenga daraja la Simiyu.
“Kwenye sekta ya maji tumepokea shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kujenga tanki lenye lita za ujazo milioni 5 litakalohudumia kata 14,” amesema Mhe. Kiswaga.
Amesema Rais Samia katika bajeti ya mwaka huu ametenga fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya kutoa maji Ihale, kujenga tanki lenye ujazo wa lita milioni 2 pamoja na mradi wa kuchimba visima virefu.
Katika upande wa sekta ya elimu, amesema “Tumepokea fedha kiasi cha shilingi bilioni zaidi ya 31, tumemaliza ujenzi wa sekondari za kata sasa tunaendelea kujenga sekondari za vijiji nia yetu ni kumpelekea maendeleo kwa wananchi,”
Vilevile, katika afya wilaya hiyo imepokea shilingi bilioni 10 ambapo wamekarabati na kujenga vituo vipya vya afya.
Aidha, ameshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo lake.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amepongeza Mhe. Kiswaga kwa kuandaa mkutano utakaotoa fursa kwa wananchi kuelezwa yale aliyotekeleza katika kuwaletea maendeleo.
“Kwa miaka mitatu Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeleta shilingi trilioni 5.6 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo hapa Magu,”
Mhe. Mtanda amesema baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, CCM Magu imeshinda katika vijiji 78 kati ya 82 na katika vitongoji 508, imeshinda vitongoji 484 huku akiwataka wananchi kudumisha amani mara baada ya uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Magu, Enos Kalambo amesema kuwa Rais Samia na Mbunge wao Kiswaga wamefanyakazi kubwa ya kuwaletea maendeleo katika wilaya hiyo hivyo wananchi waendelee kuwapa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.
Post A Comment: