Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimesisitiza kuwa ili kuleta tija katika maeneo ya kazi ni lazima wafanykazi watimize wajibu wao ipasavyo huku waajiri nao wakiwajibika kutimiza haki za watumishi wao kulingana na makubaliano katika mikataba yao.


Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu TUGHE kwa mwaka 2024, uliofanyika leo Jumanne tarehe 17/12/2024 Jijini Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Joel Kaminyoge ameeleza kuwa endapo kila upande yaani mwajiri na mfanyakazi utatimiza wajibu wake itasaidia kufanya sehemu za kazi kuwa salama na kupelekea kukua kwa uzalishaji na hatimaye kufikia malengo yanayokusudiwa.

Sambamba na wito huo, Cde. Kaminyoge alieleza kufurahishwa kwake na hatua kubwa ambazo Chama imepiga ambapo sasa kinatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake na kutaja baadhi ya maeneo kama vile huduma za ushauri wa kisheria kwa wanachama, kuimarisha mahusiano na wadau, uwekezaji katika maeneo mbalimbali ndani ya Chama pamoja na kusimamia maslahi ya watumishi nchini.

Naye Katibu Mkuu wa TUGHE, Cde. Hery Mkunda ameeleza kuwa Chama kinapoadhimisha Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, kinajivunia kuwa mstari wa mbele katika kusikiliza kero za wafanyakazi hususani wanachama wao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau na kutaja mfano wa Migogoro ambayo inapokuwa inaibuka kati ya Wafanyakazi na Waajiri wake TUGHE imekuwa ikitoka Mstari wa mbele kuhakikisha suluhisho linapatikana.

BARAZA KUU LASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA UJENZI WA JENGO LA TUGHE JIJINI DODOMA

Mapema leo kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Baraza kuu, historia mpya iliandikwa kwa tukio la utiaji sani wa Mkataba wa ujenzi wa jengo la Kitega Uchumi la TUGHE sambamba na kumkabidhi mkandarasi eneo la ujenzi (kiwanja) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni jijini Dodoma

Hafla hio fupi imehudhuriwa na Wajumbe wote wa Baraza Kuu la TUGHE wakiongozwa na Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Joel Kaminyoge aliyeambatana na Viongozi wengine wa Kitaifa wa Chama, Watendaji, Viongozi Wastaafu, Wataalamu wa Ujenzi pamoja na Mkandarasi aliyepewa kazi ya Ujenzi wa Jengo hilo litakalokuwa na Ofisi za Makao Makuu ya Chama pamoja sehemu ya Hoteli ya kisasa ambapo itakapokamilika itakuwa ni sehemu ya Kitega Uchumi kitakachoongeza mapato ya Chama.

Mkutano huo wa siku mbili wa Baraza Kuu TUGHE umefunguliwa rasmi leo ambapo ulifuatiwa na Kikao cha Kamati ya Wanawake Baraza. Katika hatus nyingine TUGHE ilitumia Mkutano huo wa Baraza Kuu kufanya Tukio la Uzinduzi Rasmi wa Kitambulisho cha Mwanachama wa TUGHE ambavyo vinatarajia kuanza kusambazwa kwa wanachama wote wa TUGHE.




Share To:

Post A Comment: