Na Benny Mwaipaja, Baku, Azerbaijan
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa wito kwa Serikali, Sekta Binafsi na Washirika wa maendeleo kuunga mkono agenda ya kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya watu waishio Barani Afrika.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo wakati akifunga mkutano uliojadili umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, pembezoni mwa Mkutano
wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko yaTabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.
Alisema kuwa ni muhimu kwa nchi za Afrika kutekeleza sera zinazochochea kasi ya matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia na kutenga fedha za kutosha kuisadia jamii hususan iliyoathirika zaidi na athari hasi ya mabadiliko ya tabianchi.
“Ni muhiu kujenga ushirikiano unaolenga kuongeza ujuzi na utaalam ili kuhakikisha kuwa suluhisho la changamoto ya matumizi duni ya teknolojia ya kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia inapatiwa ufumbuzi wa kudumu” alisema Dkt. Nchemba kwa niaba ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango
Dkt. Nchemba alilisisitiza umuhimu wa wadau wote kushirikiana ili kuweka mazingira wezeshi ya mipango ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kujenga mustakabari na kesho iliyobora kote Barani Afrika.
Mkutano huo wa nishati safi ya kupikia uliandaliwa na Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Tume ya Nishati Afrika (AFREC) uliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-29) unaofanyika katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan.
Zaidi wa watu elfu 50, wakiwemo wanadiplomasia kutoka zaidi ya nchi 200 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanakutana katika Jiji la Baku, nchini Azerbaijan wakijadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutafuta vyanzo vya fedha za uhakika za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Post A Comment: