Na Denis Chambi , Tanga.

 SERIKALI Mkoani Tanga imewatahadharisha watendaji na watumishi wote waliopewa majukumu ya kusimamia miradi inayofadhiliwa na wadau mbalimbali kutokuitumia kama kitega uchumi kwa manufaa yao binafsi huku ikiwa haikamiliki na kuleta matokeo chanya kama ilivyotarajiwa.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Handeni Albert Msando wakati akizindua mradi wa Green and Smart City SASA Program kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani uliofadhiliwa na Serikali ya Umoja wa ulaya ambao una lengo la kuboresha mazingira yawe katika hali ya usafi, kuzigeuza takangumu kuwa fursa kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu kama chanzo cha kujipatia kiipato.

Mradi huo ambao unatekelezwa katika Mikoa ya Tanga kupitia Halmashauri ya Jiji la Tanga , Mkoa wa Mwanza pamoja na Pemba utahusisha pia ujenzi wa masoko ya Kasera na Mgandini yaliyopo jijini hapa  ambapo utatekelezwa kwa muda wa miaka minne ukigharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Billion 200.

"Kumekuwa na tabia au kasumba kwenye miradi kama hii fedha zinakuja na ni nyingi kutoka kwa wafadhili lakini baada ya miaka miwili au mitatu wafadhili wakiondoka unakuta sifuri hakuna muendelezo wote, kwa niaba ya Mkuu wa mkoa sitegemei kama mradi huu utakuwa ni sawa na miradi mwingine" 

"Fedha za wafadhili zimeletwa kwetu kwaajili ya kutupa matokeo nitoe rai kwa wale wote ambao wanaosimamia mradi huu na kuhakikisha kwamba matokeo yanapatikana wajitoe , wawe wabunifu kusiwe na ujanja ujanja wa kutengeneza posho , mazingira ya kitaka kufaidika wewe binafsi nipigie mstari kabisa kwamba yeyote atakayekwenda kuchezea mradi huu hatutaweza kumvumilia hata kidogo" alisisitiza Msando.

Aidha Msando amewataka wanufaika wa mradi huo kuitumia vyema nafasi hiyo kwa ili waweze kunufaika kiuchumi ambapo watapata ujuzi wa kuzalisha na kutengeneza bidhaa mbalimbali baada ya kupatiwa mafunzo.

"Huu ni mradi wa muda mrefu na ni wa muhimu sana niwasihi sana wale wote ambao wanashiriki kwenye mradi huu ni lazima wa uangalie kama fursa endelevu wasishiriki tu kwa sababu imetokea nafasi bali ni lazima washiriki kikamilifu kwaajili ya kupata maendeleo endelevu" alisema Msando. 

Awali akizungumza meneja wa mradi huo wa Green Smart Cities Martino Vinch amesema kuwa kupiyltia mradi huo wameona kuna haja ya kuboresha mazingira hasa katika maeneo yenye mkusanyiko ambapo inaweza kutoka mlipuko wa magojwa na madhara mbalimbali ambapo shirika hilo litaweza kujenga miundombinu ya masoko ya Mgandini na Kasera hatua ambayo pia itaongeza kipato kwa wananchi hususani wafanyabiashara.

Ameongeza kuwa suala la uwepo wa Takangumu katika mazingira linaweza kuleta athari mbalimbali hususani katika nyakati za mvua ambapo mitaro inayopitisha maji imekuwa ikiziba na kupelekea mlundikano wa taka taka jambo ambalo linaweza kuleta athari kwa kuliona hilo wadau hao wameamua kutoa elimu kwa jamii kuzitumia Takangumu kuzigeuza kuwa fursa.

"Idadi ya watu inazidi kuongezeka hivyo katika mradi huu kwa kushirikiana na mashirika ambayo tunafanya nayo kazi kwenye mradi huu tunahitaji kuliweka Jiji la Tanga safi kwa upande wa maji na mazingira kuzibadilisha taka kuwa fursa ili kuwasaidia wananchi kiuchumi , tutajenga pia miundombinu katika masoko ya Mgandini na Kasera hivyo tunahitaji kulifanya Jiji la Tanga kuwa la mfano"

Kwa upande wake Msimamizi wa utekelezaji wa wa Green and Smart Cities SASA katika mikoa ya Tanga na Mwanza Fred Lerise kutoka shirika la German Development Cooperation 'GIZ' amesema kuwa katika kuhakikisha wanaijengea jamii uwezo wa Kupambana na mabadiliko ya tabianchi wamejipanga kutoa Elimu kwa wananchi ili kuondokana na madhara ambayo yanaweza kutoka baadaye na kuleta athari.

"Majukumu yetu kwenye huu mradi ni kuleta uzoefu kwa wanajamii kwa kuwajengea uwezo katika Kupambana na mabadiliko ya tabianchi , suala la tabianchi ni jambo kubwa hasa kwa nchi yetu kwa upande wa mafuriko, mvua zisizotabirika na pia ongezeko la joto ambalo kwa mji wa Tanga limeonekana kwamba ni tatizo"

Aidha aliongeza kuwa kwa kushirikiana na Serikali kupitia wizara ya maji wameweza kuanziaha mfumo rasmi wa kuwawezesha wananchi kupata huduma mtandao ambapo wanaweza kupata huduma hiyo kupitia mfumo wa mtandao ambapo shirika hilo linafanya kazi kwa karibu kwa kuahirikiana na mamlaka za maji Tanga , Mwanza pamoja na bonde la mto Pangani.

"Tunafanya kazi na wizara ya maji tumesaidia katika masuala mtandao kuweza kuhakikisha kwamba rasilimali za maji zinatumika vizuri tuna mfumo wa maji ambapo watumia maji wataweza kuomba kibali cha matumizi kupitia mtandao hautahitaji kwenda ofisi kupeleka taarifa mfumo huo unasaidia kusimamia viwanda katika usimamizi wa maji taka"

"Kuna suala la taka ngumu ambazo zisipodhibitiwa zinaweza kuziba mitaro hasa nyakati za mvya kwahiyo tunaangalia suala la usimamizi wa Taka ngumu tunajengea uwezo jamii kuweza kumtambua fursa zilizopo katika kutenganisha taka kuweza kuzifanya na kuzigeuza kuwa fursa ziweze kutumika tena au kuziuza".



Share To:

Post A Comment: