Serikali ya Jamhuri ya Malawi imeahidi kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili wagonjwa wa moyo waliopo nchini humo hasa watoto kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Mhe. Khumbize Kandodo Chiponda alipotembelea taasisi hiyo kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Mhe. waziri Chiponda ambaye pia kitaaluma ni mfamasia alisema ameridhika na huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa kwani ameona vifaa vya kisasa vya matibabu ya moyo, amekutana na wataalamu wabobezi ambao wanatibu moyo na kuipongeza JKCI kwa kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo ya moyo.
“Nimefurahi sana kufika hapa nimeona uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali yenu pamoja na huduma inayotolewa ni jambo la kufurahi na kushangaa kuona huduma hii inapatikana Afrika tena katika nchi jirani ya Tanzania, tukirudi nyumbani tutaona namna ya kuwa na makubaliano na taasisi hii ili wagonjwa wetu waje kutibiwa hapa hasa watoto”.
“Ninawashukuru wataalamu wa taasisi hii kwani mmekuwa mkiwahudumia wagonjwa kutoka nchini Malawi ninawaomba mzidi kuwahudumia kwani tunahitaji msaada wenu tunafurahi kuona baada ya kupata matibabu wagonjwa wanarudi nyumbani wakiwa na furaha. Pia ninawaomba mje nchini kwetu japo kwa wiki mbili kufanya kambi za matibabu ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya moyo”, alisema waziri Chiponda.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo Dkt. Angela Muhozya alimshukuru waziri huyo kwa kutembelea JKCI na kusema kuwa watahakikisha wanatoa huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa Malawi wenye matatizo hayo.
Dkt. Angela alisema mwaka jana wataalamu wa taasisi hiyo walikwenda nchini Malawi katika hospitali ya Queen Elizabeth iliyopo katika nchi hiyo kufanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo ambapo waliona watu 724 kati ya hao waliokuwa na matatizo ya moyo walikuwa 537.
“Taasisi yetu imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika hasa zile tunazopakana nazo mipaka ikiwemo ya Malawi hadi sasa tumeona wagonjwa 33 kutoka nchini hiyo ambapo watu wazima walikuwa 22 na watoto 11”.
“Licha ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo taasisi yetu pia inatoa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wa afya, ninawaomba muwatume madaktari na wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba vya moyo waje kujifunza jinsi ya kuwahudumia wagonjwa wa moyo pamoja na kutumia vifaa hivyo”, alisema Dkt.Angela.
Kwa upande wake balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Agnes Kayola alisema wamekuwa wakitumia majukwaa mbalimbali kutangaza diplomasia ya uchumi inayojumuisha mipango ya kuinufaisha nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.
“Wenzetu kutoka nchini Malawi wamekuja Tanzania kuhudhuria mkutano wa MERCK Foundation nasi tukaona tutumie nafasi hii kuwaleta JKCI ili waone huduma za matibabu ya moyo tunazozitoa, wamefika hapa wameziona na kuzitambua hii itasaidia kuwashawishi wamalawi kuja kutibiwa moyo nchini kwetu”, alisema Mhe. Balozi Agnes.
Mhe. Balozi Agnes alisema Tanzania imepiga hatua katika sekta ya afya kwani wananchi wanapata kwa karibu huduma za kibingwa za matibabu wao kama ubalozi wataendelea kuwashawishi wamalawi kuja kutumia huduma za matibabu ya zilizopo nchini.
Post A Comment: