Sauti ya mtoto Maliki Hashimu (6), mkazi wa Goba, Jijini Dar es Salaam imerejea kwa 100% baada ya kukamilisha hatua zote za matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na majeraha makubwa aliyopata yaliyotokana na kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni Julai mwaka huu, kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kusababisha ashindwe kupumua, kuongea, kupata maumivu pamoja na kupoteza damu nyingi.  

Akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya kitabibu ya mtoto huyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema matibabu ya mtoto Maliki yamefanyika hatua kwa hatua na watalaam wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata mtoto huyo kwa kurejesha kila kilichokuwa kimepata hitilafu kwenye shingo yake na kwamba sasa yupo salama kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida.
Naye Mbobezi wa Upasuaji Shingo na Mkuu wa Idara ya Pua Koo na Maskio, Dkt. Aslam Nkya, amesema mtoto huyo alipofikishwa hospitalini alikua na jeraha mbele ya shingo, lililoharibu tezi la mbele liitwalo (thyroid gland) baada ya kukatwa katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi, kupata maumivu makali sehemu iitwayo (trachea) ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iweze kwenda kwenye sanduku la sauti kumuwezesha kuhema na kuongea kwa mantiki ambavyo vyote vimerejeshwa katika hali yake ya kawaida.
Mama mzazi wa mtoto huyo Bi. Shani Charles kipekee amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa gharama za matibabu ya mtoto huyo kiasi cha TZS. 15Mil, watoa huduma wote wa Hospitali walioshiriki kumuhudumia mpaka hatua aliyofikia leo kuruhusiwa moja kwa moja, jamii ya watanzania walioguswa na tukio hilo pamoja na vyombo vya habari vilivyofuatilia kwa karibu jambo hilo.


Share To:

Post A Comment: