Wananchi wa Mkoa wa Songwe pamoja na viongozi wa vyama vya siasa wametakiwa kufanya kampeni za kistaarabu na kushiriki uchaguzi kwa amani kipindi cha kampeni na siku yenyewe ya uchanguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Kauli hiyo imetolewa Novemba 07, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga alipokuwa kituo cha radio Vwawa Fm 103.7 wakati akitoa elimu juu ya madhara ya vurugu katika kipindi cha kampeni na uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

"Fanyeni kampeni za amani bila kufanya au kuleta vurugu kwani jukumu la ulinzi ni letu sote, matarajio yangu kampeni na uchaguzi utakuwa wa amani na utulivu pia nategemea kupitia wagombea na vyama husika mtaongea na wafuasi wenu kutokufanya vurugu ili uchaguzi uwe wa amani na utulivu" alisema Kamanda Senga.

Kamanda Senga aliwataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuacha tabia ya kuingia kwenye mikumbo ya kushawishiwa ili wafanye fujo na vurugu katika kuelekea kipindi cha kampeni kisha uchaguzi kwani Jeshi la Polisi litachukua hatua kwa mtu, watu au kikundi chochote kitakachopanga au kufanya vurugu.

Kamanda Senga aliongeza kuwa, Jeshi hilo halitakuwa tayari kuona chama chochote cha siasa kikifanya mikusanyiko au maandamano yasiyo na kibali na ifikapo kipindi cha kampeni kuzingatia muda uliopangwa na kuacha kufanya mikusajiko isiyokuwa na tija ili uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike kwa amani.

Vilevile, Kamanda Senga alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuachana na imani za kishirikina ambazo zinaweza kusababisha migogoro na vifo katika jamii, pia aliwaomba viongozi wa dini kukemea vitendo hivyo wanapokuwa katika nyumba za ibada ili kupunguza madhara katika jamii.

Kwa upande mwingine Kamanda Senga alisema kuwa katika kuelekea kipindi hiki cha mwisho wa mwaka kikiambatana na uchaguzi wazazi wanajukumu la kuendelea kuwa karibu sana na watoto wao ili kujua yanayowasibu kwa lengo la kuwalinda wasifanyiwe unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.

Sambamba na hayo, Kamanda Senga alitoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji dhidi ya watoto ili yaweze kutokomezwa mkoani humo na jamii ya wana Songwe iendelee kuwa salama kwa manufaa ya nchi na ustawi wa familia zao.

Share To:

Post A Comment: