WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wakubwa na wadogo kwenye sekta ya madini ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa tija na kusaidia kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.

Amesema lengo ni kuwezesha sekta hiyo inaendelea kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuhakikisha inachangia zaidi ya asilimia 10 katika pato la Taifa ifikapo 2025.

“Hii ni pamoja na kuendelea kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege ili kusaidia shughuli za madini kufanyika kwa tija na kwa gharama nafuu.“

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo  (Jumanne, Novemba 19, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania unaofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Amesema lengo la mkutano huo ni pamoja na kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi wenye rasilimali na teknolojia za kisasa, hivyo utasaidia kuongeza mtaji na teknolojia mpya, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi. Pia, mkutano huo unalenga kukuza usimamizi bora wa rasilimali madini kwa manufaa ya Taifa.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 mwaka 2023. “Ni matumaini yangu kuwa ifikapo mwaka 2025, Sekta ya Madini itafikia lengo la mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa.“

Aidha, Waziri Mkuu amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu nchini kutekeleza takwa la kisheria la kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupitia viwanda husika ili kuisaidia Serikali kutimiza dhamira yake njema ya kuwa na akiba ya dhahabu;

Katia hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango wa wachimbaji wadogo katika uchumi. Hivyo, Serikali inahakikisha inawawezesha kwa kutoa maeneo ya uchimbaji, huduma za utafiti na uchorongaji, pamoja na umeme kwenye migodi yao, ambapo hadi kufikia Septemba 2024, zaidi ya migodi 350 ya wachimbaji wadogo imeunganishwa na gridi ya Taifa.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeanzisha ziara za kimafunzo kwa wachimbaji wadogo, ikishirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA). Mwaka 2023, wachimbaji 95 walitembelea China kujifunza teknolojia ya kisasa na kutafuta masoko ya madini yao.

Kwa Upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 maduhuli yenye thamani ya shilingi bilioni 161 yalikusanywa na kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. “Mwaka huu wa fedha 2024/2025 kuanzia Julai Mosi, sekta ya madini ilichangia kwenye mfuko mkuu wa Serikali shilingi bilioni 392, lengo letu ni kufikia shilingi trilioni moja ifikapo Juni 2025.”

Aidha, Mheshimiwa Mavunde amesema kuwa sekta ya madini imeongeza mchango wake katika pato la Taifa kutoka asilimia 9.3 hadi asilimia 11.3 hivi sasa.

Share To:

Post A Comment: