#KAZIINAONGEA

 

Tanzania imewaalika wawekezaji kutoka nje ya nchi, kuja kuwekeza katika Sekta ya Nishati nchini kwa kuwa Tanzania zipo fursa mbalimbali.


Mwaliko huo umetolewa katika Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaoendelea nchini Afrika Kusini kupitia Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi.


Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu, tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani,  ambae amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Sekta ya Nishati imekuwa kwa kasi na kuweza kutoa fursa za Uwekezaji nchini.


Miongoni mwa fursa zilizopo katika sekta hiyo ni vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, miundombinu ya mafuta na gesi, miradi ya Nishati Jadidifu na viwanda vya Petrokemikali.

 

Kwa upande wa vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia tayari Wizara ya Nishati imekamilisha maandalizi muhimu kuelekea tukio la uzinduzi wa duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia vilivyo wazi ambao utaanza rasmi Machi, 2025 wakati wa Mkutano na Maonesho ya Petroli ya Afrika Mashariki utakaofanyika Jijini Dar es Salaam.

 

Katika mkutano huo, Tanzania itanadi Jumla  ya vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini ambapo kati ya vitalu hivyo, vitalu 23 vipo eneo la Baharini na vitatu vipo eneo la Ziwa Tanganyika.

 

Pamoja na vitalu hivyo, ipo fursa kwa wawekezaji kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuendeleza vitalu vya Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi, vitalu ambavyo TPDC imeendelea kuvifanyia utafiti wa mafuta na gesi asilia.

 

Vitalu vyote vitakavyowekwa sokoni ni vile vinavyoendeshwa na TPDC kwa lengo la wawekezaji kuona na kushiriki mnada huo kikamilifu.

 

Maeneo mengine ya uwekezaji katika sekta ya gesi asilia ni uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari na viwanda vya petrokemikali kwa kutumia gesi asilia.

 

Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya Uwekezaji nchini na kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), hivyo Tanzania ni sehemu sahihi kwa Uwekezaji.


#KAZIINAONGEA

Share To:

Post A Comment: