Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi, imetoa tahadhari kwa watumishi wa mizani pamoja na wasafirishaji wa Kanda ya Magharibi, inayojumuisha mikoa ya Tabora, Kigoma, Rukwa na Katavi, kuhusu utoaji na upokeaji wa rushwa ya aina mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Leonard Minja, alipozungumza katika mafunzo ya madhara ya rushwa mahala pa kazi yaliyofanyika kwa ushirikiano wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wizara ya Ujenzi.

Bw. Minja amesema kuwa amewakumbusha watumishi wa mizani na wasafirishaji kuwa rushwa inaathiri utoaji wa huduma na shughuli za maendeleo, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa uaminifu, wakiwasaidia serikali kudhibiti mianya ya rushwa.

Aidha, ametoa wito kwa wafanyakazi wa mizani kubadilisha mtazamo na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kutegemea manufaa binafsi, kwani hii inaweza kuwaleta katika vitendo vya rushwa kwa kushirikiana na wasafirishaji.

Amesisitiza kuwa vitendo vya rushwa vinavyojirudia vinavuruga utoaji wa huduma kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi.

“Rushwa ikikithiri itachangia uharibifu wa miundombinu ya barabara kutokana na magari ya mizigo kupakia mizigo kupita kiasi,” alisema Bw. Minja na kuongeza kuwa, “Mkiruhusu rushwa mtafanya wananchi na wapokea huduma kuichukia serikali na kuizungumzia vibaya, na hii itasababisha kuathiri shughuli za maendeleo, na hata kufanya miundombinu kutokuwa salama.”

Hatahivyo, amesisitiza kuwa jukumu la kupambana na rushwa haliko kwa TAKUKURU pekee, bali makundi mbalimbali yanapaswa kushirikishwa na kuwa mstari wa mbele katika kuzuia vitendo vya rushwa.

Share To:

Post A Comment: