Serikali pamoja na wadau wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu nchini wameazimia kutekeleza mpango harakishi na shirikishi wa kuibua wagonjwa wa Kifua kikuu na Ukoma nchini.

Wakiongea kwenye kikao cha siku tatu kinachoendelea jijini Dodoma washiriki wa kikao wamebainisha kuwa mpango huu unakuja kwa dharura ili kuziba pengo la wagonjwa ambao hawakuweza kupatikana katika kipindi cha Januari-Septemba, 2024 kutokana na sababu mbalimbali.

Mpango huo utakaotekelezwa kwa kampeni utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapata wagonjwa waliokosekana kwa kipindi hicho.

Akizungumza wakati wa majadiliano hayo Mtaalam Mshauri Dkt. Emmanuel Matechi kutoka Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma Wizara ya Afya amesema mpango huo umelenga kutafuta wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya vyenye idadi kubwa ya wahisiwa wa Kifua Kikuu. 

Vile vile kampeni hii itifikia jamii kupitia watoa huduma wa ngazi ya jamii ambapo wagonjwa na wahisiwa watahudumiwa na pia makundi yote yalio katika hatari ya kupata Kifua Kikuu kama wachimbaji wa madini, wafungwa, wanaoishi na VVU pamoja na watu wanaoishi katika maeneo yenye misongamano yatafikiwa.

“Tumejipanga kuyafikia makundi yote yaliyo katika hatari ya kuambukizwa Kifua Kikuu ili kuwapata wagonjwa wote wa TB na kuwaweka kwenye matibabu na kuzuia kueneo kwa ugonjwa huu sambamba na kufikia malengo ya nchi na ya dunia” alisema Dkt. Matechi

Akichangia mada wakati wa Majadailiano Happiness Msengi Afisa Kiungo wa Kifua Kikuu kutoka Wizara ya Mawasiliano amesema elimu inabidi iwafikie wadau muhimu ambao kwa namna moja wanaushawishi ndani ya jamii

"Tukiwashirikisha viongozi wa dini na wao wakalibeba jambo hili kutokana na wao kuwa na ushawishi wakiliongea kwenye nyumba za ibada ajenda yetu itafanikiwa" amesema Bi. Msengi 

Aidha, akizungumza katika kikao hicho Dkt. Mageda Kihulya kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kama wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwenye utekelezaji kila Mkoa uwe na ramani ya kazi na namna watakavyo tekeleza.

Zoezi hili limepangwa kufanyika katika mikoa tisa nchini ambayo inakabiliwa na tatizo kubwa la ugonjwa wa kifua Kikuu.


Share To:

Post A Comment: