Na: Farida Ramadhan na Josephine Majura WF, Dodoma

Serikali inatengeneza mfumo wa kidigitali utakaowawezesha Wastaafu kujihakiki wenyewe (Self verification) kupitia simu zao za mkononi au kwa kutumia huduma za kibenki ili kuwapunguzia Wastaafu gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwenda kuhakikiwa. 

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Mhe. Amandus Julius Chinguile, aliyehoji kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa Wastaafu kuhakikiwa kwenye Halmashauri au Kata badala ya utaratibu wa sasa wa kuhakikiwa Mikoani.

Mhe. Chande alisema uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina umekuwa ukifanyika katika ngazi ya Halmashauri, hata hivyo, ili kuwapunguzia Wastaafu gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kwenda kuhakikiwa, Serikali inatengeneza mfumo wa kidigitali utakaowawezesha Wastaafu kujihakiki wenyewe.

Alisema baada ya kukamilika kwa taratibu zote, Wastaafu watapewa elimu ya jinsi ya kujihakiki wenyewe na watatangaziwa siku ya kuanza kujihakiki.

Katika hatua nyengine, Mhe. Chande aliliambia Bunge kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha uchumi wa maeneo yote ya nchi ili kuweka mazingira yatakayovutia benki na taasisi za fedha kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini.

Alitoa maelezo hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingwi, Mhe. Omar Issa Kombo, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga Benki za NMB na CRDB kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni.

Mhe. Chande alisema kuwa uamuzi wa kufungua matawi ya benki hufanywa na benki yenyewe ambapo kabla ya kufanya uamuzi huo, benki hufanya upembuzi yakinifu ukiwa na lengo la kuangalia kama kuna uwepo wa biashara ya kutosha ambayo italetea faida.

“Mabenki yakishafanya upembuzi yakinifu katika sehemu husika huwasilisha uamuzi/pendekezo lao Benki Kuu ya Tanzania”, alisema Mhe. Chande.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Benki Kuu haina kizuizi chochote katika suala la mabenki kufungua matawi, kama benki husika itatimiza masharti yote ya kufungua matawi kama yalivyoainishwa katika kanuni namba 31 ya Kanuni za Utoaji Leseni za Mabenki na Taasisi za Fedha za Mwaka 2014.

Mhe. Chande alibainisha kuwa Benki za NMB na CRDB hazina matawi kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Micheweni lakini , wananchi wa Wilaya ya Micheweni wanapata huduma za kibenki kutoka benki za CRDB na NMB kupitia mawakala wa benki, ambapo hadi kufikia Oktoba 2024, kulikuwa na jumla ya mawakala 4 wa Benki ya CRDB na 14 wa Benki ya NMB wanaotoa huduma za kibenki katika Wilaya hiyo.
Share To:

Post A Comment: