Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanzisha mpango mkakati wa kuhakikisha mifumo yote ya afya inasomana ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kutumia mifumo na tekinolojia za kisasa ambazo zinatoa suluhisho la tiba kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya kansa ya matiti pamoja na kansa ya shingo ya kizazi kwa wanawake.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Novemba 14, 2024 wakati akifungua kongamano la Nne la 'Tanzania Digital Health and Innovation forum 2024' linalofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila Kibamba Jijini Dar es Salaam.
Amesema, maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Sekta ya Afya inatumia mifumo na tekinolojia ya kisasa katika kutoa tiba kwa wagonjwa ambazo zinatoa suluhisho muafaka katika kila aina ya changamoto kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa.
"Sisi kama Wizara ya Afya kwa maelekezo ya Mhe. Rais tumeanzisha mpango mkakati wa kuhakikisha tunafanya mifumo yote ya afya isomane nchini, kwakuwa ulimwengu wa sasa lazima twende kwenye ubunifu wa vifaa tiba ambavyo vitatusaidia kutatua changamoto kwenye sekta ya afya," amesema Mhe. Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika Sekta ya Afya ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ametoa zaidi ya Shilingi Trilioni 6.2 ili kuboresha miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba ikiwemo vya uchunguzi pamoja na upatikanaji wa dawa.
Amesema, Chuo kikuu cha MUHAS ni kati ya vyuo vikuu vinavyotoa madaktari wabobezi na wenye ujuzi wa hali ya juu katika kutoa tiba nchini, kwa sasa Serikali imejikita kutoa elimu ya ubunifu wa vifaa tiba, ubunifu wa mifumo itakayosaidia kuunganisha mnyororo wa Sekta ya Afya kuanzia kwenye kutibu.
Aidha, Waziri Mhagama amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka ikiwemo magonjwa ya figo, kansa, moyo, kisukari ambayo ukitaka kupambana nayo lazima kuyafanyia uchunguzi wa tekinolojia ya kisasa na kwa haraka ili tatizo lisiongezeke.
"Nimefurahi sana baada ya kupita kwenye haya maonesho, nimegundua kwamba tatizo la ongezeko la kansa ni kwa sababu Serikali imeendelea kuwekeza na kugundua wagonjwa ambao wanadalili zile za awali, wakiwemo wenye kansa ya shingo ya kizazi pamoja na kansa ya matiti kwa kina mama na kina baba," amesema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na chuo hicho pamoja na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwa kutembelea chuo hicho.
Post A Comment: