Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika kurejesha uhuru wa Habari nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya Reporters Without Borders (RSF) hadi kufikia mwaka 2023 Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 143 ya viwango vya Uhuru wa Habari duniani.
Hata hivyo juhudi za kisera na sheria zilizochukuliwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kama vile kurekebisha baadhi ya sheria za vyombo vya habari na kuruhusu vyombo vilivyofungiwa kurejea hewani, zimeisaidia Tanzania kupanda hadi nafasi ya 97 kwa mwaka huu.
Hatua hii inaifanya Tanzania sasa kuwa ya kwanza kwa Uhuru wa vyombo vya Habari kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha upatikanaji wa Habari na uhuru wa kutoa maoni kwa Watanzania umekuwa ni wa kiwango cha kuridhisha.
Hali hiyo imeondoa malalamiko ya kuminywa kwa haki hiyo ya kupata taarifa.
Rais Samia hajaishia katika kuinua uhuru wa Habari nchini, pia amepambana kuinua uchumi wa vyombo vya Habari na wanahabari.
Mara kadhaa Rais Samia amekuwa akizitaka Taasisi na Idara mbali mbali za serikali yake, kulipa madeni yote wanayodaiwa na vyombo vya habari nchini kulingana na mikataba ya kazi waliyoingia kabla ya Desemba 24, mwaka huu.
Hivi karibuni Rais Samia amerejea agizo hilo wakati akifungua Kongamano la pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari nchini, lililokuwa likijadili masuala mbali mbali na kutoa maelekezo ya madeni ya vyombo vya Habari kulipwa.
Rais pia ameyagusa maslahi ya mwandishi mmoja mmoja, ambapo alivifungulia baadhi ya vyombo vya Habari vilivyofungiwa yakiwemo magazeti, ambayo kufungiwa kwake kulisababisha baadhi ya waandishi kupoteza ajira.
Ikumbukwe kuwa, kwa kipindi kirefu, Waandishi wa Habari wamekuwa wakifanyakazi katika mazingira magumu ikiwemo kutolipwa stahiki zao pamoja na kukosa uhuru katika kufanya kazi zao.
Dhamira ya Rais Samia, imekuwa chachu hata kwa viongozi wengine kuhakikisha wanasimamia kile alichokiasisi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yeye ni miongoni mwao na amesema Serikali imeandaa mkakati wa Mawasiliano ya Taifa ili kuhakikisha wadau katika ngazi zote wanapata taarifa za kutosha na wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi na kuimarisha mawasiliano ya Serikali.
Aidha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetakiwa kuandaa utaratibu wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa Waandishi wa Habari za mitandaoni ili kuwajengea uwezo wa kufanyakazi zao kwa kuzingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania. Na kuendelea kusimamizi Sekta ya Habari ipasavyo kwa kuzingatia maadili na kujiepusha na uchapishaji wa taarifa na picha zinazochochea uvunjaji wa maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Katika kuthibitisha umuhimu wa sekta ya habari nchini, naye Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Adolf Mkenda amesema kuwa, Sekta ya habari ni muhimu na inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi, hivyo serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari katika kuboresha sekta muhimu ikiwemo ya elimu. Dkt. Mkenda pia amevipongeza vyombo vya habari na waandishi kwa ujumla kwa kuweza kusambaza habari kwa wakati na haraka zaidi ili jamii iweze kutambua juhudi zinazofanywa na serikali nchini.
Amethibitisha hayo Novemba 1,2024 katika Mkutano Mkuu wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) mkoani Singida ambapo viongozi wa klabu za Waandishi wa Habari kutoka mikoa 28 nchini wamekutana kujadili maendeleo ya taasisi yao.
#KAZIINAONGEA
Post A Comment: