Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Khalid Massa amesema Mpango wa Taifa wa Afya na lishe shuleni ni muhimu katika kuimarisha afya za Wanafunzi.
Dkt. Massa amebainisha hayo leo Novemba 13, 2024 katika Kikao cha Kupitia Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji ( Operation Plan) Afya na Lishe Shuleni wa Mwaka 2025-2029 kilichofanyika katika Ofisi za Idara ya Kinga zilizopo Itega Jijini Dodoma.
Aidha, Dkt. Massa amesema Mpango huo umekuja kwa muda mwafaka katika kuimarisha Afya na Lishe za wanafunzi katika shule.
"Kama mnavyofahamu afya na lishe za wanafunzi ni jambo la msingi katika kuimarisha Afya za Wanafunzi hivyo Mpango huu umekuja kwa muda mwafaka"amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesema jukumu la Elimu ya Afya ni kuelimisha hivyo kupitia Mpango huo utarahisisha kuwafikia walengwa kupata elimu ya Afya sahihi.
"Mpango huu una tija kubwa katika kufikisha elimu sahihi kwa wanafunzi, walimu na wazazi "amesema.
Akiwasilisha Mpango huo, Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Afya na Lishe Shuleni kutoka Wizara ya Afya Beauty Mwambebule amesema, Mpango wa Utekelezaji wa Taifa wa Afya na Lishe kwa wanafunzi katika shule, umegusa maeneo yote muhimu ya uelimishaji kuhusu Afya na Lishe. Aidha, Mratibu alianisha maneno muhimu kuwa Nyaraka hii imeboreshwa zaidi ikiwemo kuainisha Afua mbalimbali, bajeti halisi na Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini.
Post A Comment: