Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa kiasi cha shilingi milioni 455.7 kwa ajili ya kusambaza mitungi ya gesi ipatayo 22,785 mkoani Tabora ukiwa na lengo la kuhamasisha na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini. 

Hayo yamebainishwa leo Novemba 22, 2024 na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Mha. Advera Mwijaje wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA ya mkoani humo.

Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Uyui, Urambo, Nzega, Sikonge, Kaliua, Igunga na Wilaya ya Tabora.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya amesema kuwa, suala la Nishati Safi ya Kupikia sasa ni ajenda ya kimataifa na wataibeba katika kuelimisha umma kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo kwa upana.

Dkt. Mboya ameipongeza REA kwa mradi huo na miradi mingine mbalimbali inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ikiwemo ya kufikisha umeme kwenye vijiji na vitongoji. 

"Nawapongeza REA kwa kuendelea kusambaza mitungi ya gesi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Nawapongeza pia kwa kuendelea kufikisha umeme katika maeneo mbalimbali, natoa rai kwenu kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni makubwa katika kutekeleza miradi hiyo nchini ili kuifanya kuwa na tija kwa wananchi." Amemalizia Dkt. Mboya.





Share To:

Post A Comment: