Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Tanga Mjini, Eng. Juma Hamsini, amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Jiji la Tanga, kutumia vikao rasmi katika kufanya maamuzi, badala ya kufanya mambo kienyeji kwa kufahamiana. 

Eng. Hamsini ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi hao mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuapishwa kwao, lililofanyika leo kufuatia ushindi walioupata katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana, Jumatano, Novemba 27, 2024, katika mitaa 181 ya Jiji la Tanga.

Hamsini amesema kama jambo linahusu jamii, au serikali, viongozi hao wana wajibu wa kuitisha vikao na kutatua jambo hilo ambalo litaingia kwenye kumbukumbu za vikao. 

Akizungumzia suala la usafi wa mji, Eng. Hamsini ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, amesema tayari Halmashauri ipo kwenye mpango wa kubinafsisha shughuli za uzoaji taka, na tayari wazabuni watano wamepatikana. Na hivyo amewataka viongozi hao kuhamasisha ulipaji wa ada ya uzoaji taka. 

Hamsini pia amesema Jiji lina lengo la kufunga taa za barabarani zipatazo 1500, ambapo tayari taa 300 zimeanza kufungwa na taa 1200, zitapatikana kupitia mradi wa TACTIC.

Aidha ameahidi kuwapatia mafunzo ya juma moja (wiki moja) Wenyeviti hao, ili waweze kujua majukumu yao.

Share To:

Post A Comment: