Na.Elimu ya Afya Afya kwa Umma.

Imeelezwa kuwa matokeo makubwa  ya  kuleta ufanisi kwenye sekta ya afya na uwekezaji katika eneo ka kinga na wenye msukumo mkubwa wa kuleta mabadiliko kwenye  jamii ni Wahudumu  wa Afya Ngazi ya Jamii.

Hayo yamebainishwa na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii , Wizara ya Afya Dkt. Meshack Chinyuli akizungumza  Jijini Mbeya mara baada ya ujumbe kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya ziara ya Usimamizi Shirikishi katika Chuo cha Afya  na Sayansi Shirikishi Uyole.

Dkt. Chinyuli amesema   uwekezaji wa Kinga katika Afya Ngazi ya Jamii utakuwa na matokeo makubwa.

“Kumekuwa na desturi  kwenye mifumo mingi ya afya katika nchi zetu za Afrika , kuwekeza sana kwenye maeneo ya tiba, lakini tafiti zinaoenesha kwa sasa matokeo makubwa yanatokana na kuwekeza kwenye eneo la kinga na hiyo kinga ndio asilimia 80 mnaenda kufanya Wahudumu wa afya Ngazi ya Jamii na kinga inaanzia kwenye elimu , mtu akijua vyanzo vinavyoweza kumsababisha apate magonjwa , na magonjwa yanatokea kwenye jamii na hospitalini tunaenda baada ya kuumwa, hivyo tukiimarisha mifumo ya afya ngazi ya jamii tutaipunguzia hata serikali nguvu kubwa ya kuwekeza kwenye dawa na vifaa tiba ”amesema .

Kwa upande wake mjumbe kutoka Wizara ya Afya, Mwalimu Yuster Makule  ambaye pia ni Mkufunzi kutoka Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kiomboi Mkoani Singida ametoa wito kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuwa wawakilishi wazuri kwa kuzingatia kanuni za utumishi .

“Baada ya mafunzo haya wataenda kwenye jamii ni vyema kuzingatia kanuni za kiutumishi ikiwemo kuzingatia mavazi ya heshima, lugha nzuri kwenye jamii”amesisitiza.

Kwa upande wao baadhi ya wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii akiwemo Dufe Mtawa, Gideon  Aron pamoja na Ismail Rajab wamesema watayatumia mafunzo hayo  kwa kufanya kazi kwa ufanisi katika jamii inayowazunguka ili kuleta mabadiliko chanya kwenye eneo la afya.

Kwa Upande wake Afisa kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa Clarence Mkoba amesema Taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana  na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI tangu mwanzo wa mchakato wa Mpango wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii hadi suala la mafunzo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa baadhi ya Vyuo vinavyotekeleza mafunzo hayo.

Ikumbukwe Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango   Januari  31 ,2023  huku   mikoa 10 iliyo katika awamu ya kwanza ya mpango huu ni Njombe, Mbeya, Songwe, Tabora, Kigoma, Geita, Kagera, Lindi, Mtwara na Pwani.

Hivyo, Mafunzo haya maalumu yanatolewa ndani ya vyuo vya Afya vya Serikali na binafsi.

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tamisemi inaatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya ngazi ya jamii 11,515 na yalianza Rasmi Septemba 30, 2024 ili kufanikisha azma ya Mpango Jumuishi wa wahudumu hao na kuendeleza afua jumuishi za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii.

Share To:

Post A Comment: