Ili kufanikisha malengo ya Mtanzania kuepukana na adha ya moshi unaotokana na nishati chafu ya kupikia, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amewataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kuchochea ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini. 

Ametoa wito huo leo Novemba 21, 2024 mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage.

Amesema, Rais Samia anaendelea kuipeleka ajenda ya nishati safi kimataifa ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya.

Mkuu huyo wa mkoa ameongeza kuwa, suala la Nishati Safi ya Kupikia kwa  sasa ni ajenda ya kimataifa na wataibeba katika kuelimisha umma kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwijage amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba hatua hiyo itawezekana kwa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu inayopatikana na kutumika kwa urahisi.

Aidha amesema serikali imejipanga kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wengi na tayari   kampuni ya Taifa Gas Limited imepewa jukumu la kuhudumia  wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Rukwa na watasambaza mitungi 9,765 kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.

Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Kalambo, Sumbawanga na Nkasi.

#KAZIINAONGEA

Share To:

Post A Comment: