Na Mapuli Kitina Misalaba
Ligi ya XMASS CUP, iliyoandaliwa na Makamba Mussa Lameck, inaendelea kwa kasi katika kata ya Salawe, Wilaya ya Shinyanga Vijijini. Ligi hiyo, inayojumuisha timu 16, imeendelea kuvutia mashabiki wengi wa mpira wa miguu kutoka maeneo mbalimbali.
Msimamizi wa ligi hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amesema kuwa ligi imekuwa na mwitikio mkubwa huku akieleza kuhusu mechi zilizochezwa hivi karibuni.
MECHIYA JANA: KANO FC YANG’ARA DHIDI YA MAHEMBE FC
Jana, Kano FC iliibuka mshindi kwa ushindi wa mabao mawili dhidi ya Mahembe FC, katika mechi iliyokuwa ya ushindani mkubwa.
MECHIYA LEO: COMBINE FC YASHINDA DHIDI YA SCARD ONE FC
Leo, vijana wa Combine FC, walioundwa na wanafunzi wa shule za sekondari za Salawe, walichuana vikali na timu ya Isenengeja FC (Scard One FC) kutoka Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza ambapo Combine FC wamefanikiwa kuondoka na ushindi wa goli moja, huku mashabiki wakishuhudia mchezo mzuri wa soka.
Kesho, ligi itaendelea kwa mechi kali kati ya Machongo FC na Mwabenda FC. Mashabiki wameombwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani hiyo.
Mwandaaji na mdhamini wa mashindano haya, Makamba Mussa Lameck, ametoa shukrani kwa mwitikio mkubwa wa mashabiki na wadau wa michezo ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, usalama, na nidhamu wakati wa mashindano.
“Nina furaha kubwa kuona jinsi mnavyoitikia kuja kushuhudia ligi hii. Ushirikiano wenu tangu tulipoanza mashindano haya ni wa kipekee. Naomba muendelee kushirikiana nasi hadi pale tutakapohitimisha ligi hii. Pia, ni muhimu kuimarisha usalama wetu sote na kuheshimu wachezaji; tusihusike na fujo au vurugu za aina yoyote. Ndugu zangu, kwa pamoja tunaweza kufanya makubwa. Naomba mjitokeze kwa wingi kesho kushuhudia mechi,” amesema Makamba.
Mashindano hayo yanatarajiwa kumalizika Disemba 17, 2024, ambapo fainali itachezwa katika uwanja wa Shule ya Msingi Mahngu, kijiji cha Songambele na kwamba mfumo wa mtoano utaendelea kutumika hadi hatua ya mwisho.
Ligi hii ni moja ya juhudi za Bwana Makamba Mussa Lameck, mkurugenzi wa Kampuni ya MCL inayojihusisha na biashara ya nafaka, na kwamba imelenga kuinua vipaji vya michezo katika mkoa wa Shinyanga.
Post A Comment: