Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kutofurahishwa na hatua ya Jerry Silaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ‘kukwepa’ mikutano ya kihabari.
Akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nane wa jukwaa hilo leo tarehe 7 Novemba 2024, jijini Dar es Salaam amesema, waziri huyo tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 22 Julai 2024, amealikwa katika matukio ya kihabari manne ikiwemo wa TEF, yote hajahudhuria.
“Waziri wetu huyu, sisi hatuna mambo ya kusema chini chini maana sisi tukisema chini chini wengine watafanyaje? Amealikwa kwenye mkutano wa wadau wa habari Arusha PRST hakwenda.
“Amealikwa kwenye Tuzo za Uandishi wa Habari Mahiri (EJAT), hakwenda. Nikasikia amealikwa Mbeya, tukasema basi (sisi TEF) tumpe nafasi akutane na sisi tumualike, hakuja anasema Spika amemzuia,” amesema Balile.
Balile amesema, wadau wa habari hawafurahishwi na tabia hiyo na kwamba, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ndio mchungaji tasnia ya habari.
“Sisi tunaamini kwamba, Waziri wa Habari kondoo wake ni vyombo vya habari, kwenye familia anapaswa kukaa nao mezani, wakala chakula pamoja, wakajadiliana na akaona ni mtoto yupi anakomba mboga.
“Hatufurahishwi na hatutaki kugawana mbao katikati ya bahari wala hatusemi kama anatujaribu, lakini akitaka huo mkondo sisi tupo tayari. anaweza kumuuliza Mzee Mapuli mwaka 2003,” amesema na kuongeza;
“Hatusemi kwamba tunataka kwenda huko, lakini tunaomba (Nicholaus Mkapa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) utufikishie salamu, ajue kabisa kwamba moja ya majimbo yake ni vyombo vya habari, wala hatusemi kwa ukali,” amesema.
Post A Comment: