Na Denis Chambi, Tanga
CHUO cha Dar es salaam University College of Education 'DUCE' kimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali katika mchezo wa Volleyball kwa upande wa wanawake baada ya kuwatupa nje ya mashindano hayo wapinzani wao kutoka shirika la Umeme Tanzania 'TANESCO' kwa ushindi wa seti 3-1.
Ushindi huo walioupata DUCE katika uwanja wa Mkwakwani umewatia kiburi na kujiona kuwa lolote linawezekana baada ya kuwatupa nje vigogo waliokuwa nao kwenye kundi lao ambao ni pamoja na timu za Ngorongoro, TPA, UDSM, pamoja na timu ya Ardhi.
Kocha wa timu ya volleyball kwa upande wa wanaume na wanawake Alex Pacha amewapongeza wachezaji wake ambapo licha ya kufuata na kutekeleza kile alichowaelekeza lakini pia jitihada zao binafsi zilichagiza kwa kiasi kikubwa kuibuka na ushindi huo.
"Mchezo haukuwa rahisi wachezaji wangu waliokuwa wasikivu kwenye maelekezo japo kuwa seti ya kwanza tulipoteza lakini walipambana mpaka mwisho hatimaye tumepata ushindi kuanzia seti ya pili niwapongeze sana wachezaji wangu walipambana kila mmoja kwa nafasi yake"
Macha alisema kuwa anawafahamu vyema timu ya chuo cha Mbeya University of Technology 'MUST' ambao watakutana nao kwenye hatua ya nusu fainali kusaka tiketi ya kucheza fainali katika mchezo huo ambapo ameahidi kutwaa kombe na kutimiza malengo yao kama ambavyo walipanga kwa mwaka huu.
"Tunakwenda sasa kujiandaa na nusu fainali ambayo ni hatua moja kuelekea fainali na kwa sababu tumeshamjua mpinzani wetu tunajua mbinu zake hili ni jambo zuri sana kwetu sisi ni mara ya kwanza kuingia nusu fainali lakini yeye ni mzoefu kwahiyo tunamheshimu lakini ana mapungufu machache ambayo sisi tumeshayajua na tunakwenda kuyafanyia kazi" alisema Macha.
Mwalimu wa michezo katika chuo hicho cha DUCE Juma Petter amethibitisha ule msemo usemao "kuteleza sii kuanguka ambapo baada ya kuishia hatua ya makundi mwaka 2023 walienda kukaa na kugundua ni wapi waliteleza ambapo waliyafanyia kazi madhaifu yao kisha mwaka huu kuja na nguvu mpya ambayo imewasaidia kuruka kiuzi akiwa na tumaini la kunyakua kombe katika mchezo huo.
"Haikuwa rahisi kufika hapa mashindano ya mwaka huu ni magumu sana kwa sababu timu zimeongezeka kwahiyo kama hujajiandaa vizuri huwezi kufika popote , tulijifunza mwaka jana na mwaka huu tukaona tuna haja ya kujipanga ili kufika malengo yetu.
Petter melipongeza Shirikishi la michezo ya mashirika ya umma, taasisi na makampuni binafsi 'SHIMUTA' ambao ndio waandaaji wa michezo hiyo na kwa mmwaka huu pamoja na kuongezeka kwa timu shiriki lakini pia maboresho ya miundombinu ya viwanja yamefanika Kwa kiasi kikubwa hatua ambayo inazifanya timu kufanya lolote linalowezekana ili wasirudi mikono mitupu.
"Nawapongeza sana waandaji wa SHIMUTA mwaka huu tumeona mazingira yameboreshwa kwa kiasi kikubwa timu zinacheza kwa kiwango kikubwa washiriki wanafurahia mazingira lakini na kuimarisha afya zao katika mazoezi kushindwa kufanya vizuri sii sababu ya viwanja bali ni aina ya timu pinzani utakayokutana nayo" alisema Petter.
Wakati wanawake wakifikia hutua hiyo ya nusu fainali kwa upande wa wanaume wameshindwa kufua dafu ambapo wameishia hatua ya 16 sawa na michezo ya Darts na Draft wakati huo huo wakifika husu fainali kwenye mchezo wa Karata.
Michezo zaidi ya 12 inaendelea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali hapa Mkoani Tanga kwa mwaka huu wa 2024 ikiyashirikisha mashirika ya umma, taasisi na makampuni binafsi ambapo inatarajiwa kutamatika November 24.
Post A Comment: