Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa utekelezaji wa maagizo ya serikali ya kuhakikisha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu unafanyika kwa kuzingatia utoaji wa elimu kabla ya kutoa mikopo hiyo.
Mpogolo ametoa shukrani hizo wakati wa katika Kongamano la Uelimishaji na Uhamasishaji Jamii Juu ya Uwepo wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu Sambamba na Matumizi ya Nishati Safi linalofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam tarehe 11 Novemba 2024, katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, ambapo alihudhuria kama mgeni rasmi.
"Nikupongeze Mkurugenzi Mabelya na timu yako kwa kuzunguka kwenye kata zote 36 na mitaa 159 ya Ilala ili kutoa mafunzo kwa wajasiriamali. Leo hii tunashuhudia maonesho na mafunzo ya pamoja kwa wale ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria katika maeneo mengine," amesema Mpogolo.
Mpogolo amesema kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameruhusu halmashauri hiyo kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 14 kwa vikundi vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu, hatua inayolenga kuwainua kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Dar es Salaam.
"Halmashauri yetu ya Ilala ni ya kipekee kwa kutoa mikopo mikubwa kuliko halmashauri zote nchini. Tunatoa mikopo kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya Ilala, bila kujali wanakotoka, mradi wanachangia uchumi wa eneo hili," amesisitiza Mpogolo.
Mpogolo ameeleza kwamba serikali imeamua kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo ili kuhakikisha wanajua jinsi ya kutumia fedha hizo kwa ufanisi.
"Ni muhimu kumpa mtu fedha baada ya kumfundisha namna ya kuzitumia kwa usahihi. Tunataka kuona wajasiriamali wetu wanastawi kiuchumi na kuhakikisha marejesho yanarudi kwa ajili ya kusaidia wengine," amesisitiza.
Mpogolo pia amezungumzia utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo kupitia benki, ambao umelenga kuongeza uwazi na usalama wa fedha za serikali.
"Kwa kushirikiana na taasisi za kibenki, tunahakikisha mikopo hii inatolewa kwa uwazi na ufanisi. Wapo watu wengi waliofika ofisini wakilalamika kutofahamu jinsi ya kupata mikopo. Sasa tunatoa elimu ili kuhakikisha kila mmoja anajua taratibu na sheria za mikopo," amefafanua.
Pia ametilia mkazo umuhimu wa mafunzo kuhusu usimamizi wa miradi ili wajasiriamali waweze kufanikiwa katika shughuli zao za kiuchumi. "Wapo watu wanakopa mamilioni ya fedha lakini wanashindwa kufanya marejesho kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya mikopo. Ni lazima waelewe jinsi ya kutumia mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi yenye faida," aliongeza.
Kongamano hilo linaendelea kwa siku mbili na linatarajiwa kutoa mwongozo kwa wajasiriamali kuhusu jinsi bora ya kutumia mikopo kwa maendeleo yao na ya jamii.
Post A Comment: