Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka anaongoza ujumbe wa chuo hicho katika mazungumzo na Chuo Kikuu cha Comoro ili kuanzisha ushirikiano utakaowezesha wanafunzi wa Comoro kupata mafunzo toka IAA.

Katika mazungumzo hayo yanayoendelea nchini Comoro, Profesa Sedoyeka alimjulisha mwenyeji wake, Mkuu wa Chuo cha Comoro Prof Ali Tabibu Iburoi maeneo ambayo IAA ingependa kujikita nchini Comoro kuwa ni Uhasibu, Fedha, Utawala Bora, Tehama na pia kuwa washauri katika maeneo mkakati kulingana na vipaumbele vya Serikali ya Comoro.

Hivi karibuni Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alielekeza Taasisi na Mashirika ya Umma kuangazia fursa nje ya mipaka ya Tanzania na juhudi hizo za IAA ni sehemu ya utekelezaji wa agizo hilo.

Ziara hiyo imeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro ambapo Balozi wake, Mhe. Saidi Yakubu alieleza ujumbe huo utakutana pia na Gavana wa Benki Kuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Dijitali nchini Comoro na kutembelea vitivo kadhaa vya Chuo Kikuu cha Comoro.



Share To:

Post A Comment: