Utendaji wa Bandari ya Tanga umeimarika kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na uwekezaji wa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Sh bilioni 429.1 kwa kuongeza kina cha maji kutoka mita tatu hadi mita 13, kupanua njia ya meli kugeuza, ununuzi wa vifaa vipya vya kushughulikia mizigo na upanuzi wa gati mbili katika bandari hadi upana wa mita 450
Baada ya maboresho haya, meli sasa zinaweza kutia nanga moja kwa moja kwenye gati hizo, ambayo ni mabadiliko makubwa kutoka hali ya awali ambapo meli zililazimika kufunga kwenye kina cha umbali wa kilomita 1.7 nje ya gati.
Hapo awali ilibidi kuzihudumia meli hizo kwa kutumia meli ndogo za kubebea mizigo na maboya, kutegemea meli ndogo na maboya kulisababisha TPA kutoa ada ya Dola za Kimarekani 1.3 kwa kila tani ya mizigo yote iliyosafirishwa kupitia Bandari ya Tanga, kwa sasa ada hii haipo tena kwa sababu meli ndogo na kubwa zinaweza kupewa huduma ipasavyo ndani ya bandari.
Maboresho haya pia yameimarisha utendaji kazi wa Bandari ya Tanga, yakiwezesha bandari hiyo kupakua mizigo kutoka kwa meli kubwa ndani ya siku mbili, tofauti na siku tano au zaidi zilizokuwa zinahitajika hapo awali.
Aidha Wakati wa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha wa sasa, bandari hiyo imehudumia jumla ya tani 333,643 za mizigo, ikipita lengo lake la tani 283,225 kwa asilimia 17 ikilinganishwa na tani 204,000 zilizohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha wa 2023/24.
Kwa ujumla, Bandari ya Tanga ilishughulikia tani 1,191,480 za mizigo wakati wa mwaka mzima wa fedha wa 2023/24, ikiongezeka kutoka tani 890,901 mwaka uliopita.
Post A Comment: