Mbunge wa  Vitimaalum kupitia kundi la Wanawake (UWT) Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Zaytun Swai ameanza ziara yake ya siku tatu wilayani Monduli yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wilayani humo.

Akiwa Katika ziara hiyo ametembelea Kituo cha Afya Nafco kilichopo Kata ya Lolkisare wilayani humo ambapo moja ya changamoto zilizobainishwa ni pamoja na Ukosefu wa Genereta pamoja na Wakina mama wa eneo hilo kupenda kujifungulia nyumbani badala kwenda kujifungulia  kwenye Vituo vya Afya.

Akijibu changamoto hizo Mbunge Zaytun aliahidi kutatua changamoto ya Genereta katika Kituo pamoja na kuwaomba wanaume kuhamasisha wanawake kwenda katika maeneo yao kujifungulia katika Vituo vya afya ili kupata huduma bora na kuhakikisha usalama wa maisha ya mama na mtoto.

Sambamba na hilo Mbunge Zaytun aliwataka wanawake kuhakikisha wanajitokeza kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi katika chaguzi zijazo ikiwa ni pamoja kuhamasisha jamii katika zoezi la kujiandikisha katika Daftari la kupiga kura ili kuweza kuchagua viongozi sahihi katika kutatua changamoto katika maeneo yao.

“Kwa Mkoa wetu wa Arusha zoezi la kujiandikisha katika Daftari la kupiga kura litaanza Oktoba 11 hadi 20 hivyo tujitokeze kwa wengi kwani ngazi ya serikali za mitaani ni muhimu sana katika uchaguzi na ni muhimu tuhakikishe tunachagua viongozi bora ambao wataweza kusikiliza kero zetu na kuzitafutia ufumbuzi kwa maendeleo ya jamii zetu” Ameongeza kusema Mh,Zaituni.

Katika ziara hiyo Mbunge Zaytun Swai  aligawa taulo za kike pamoja na mipira ya michezo katika Shule ya Sekondari Meserani pamoja na mashuka,sabuni,beseni kwa wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika Kituo cha Afya Nafco ili kuwapa Faraja wagonjwa na kutoa hamasa kwa wanamichezo kuendelea kushiriki vyema katika michezo Wilaya.



Share To:

Post A Comment: