Na Elinipa Lupembe.
Jumla ya watahiniwa 39,075 mkoa wa Arusha wanatarajika kufanya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2024, unaotarajia kuanza nchini leo tarehe 28 Oktoba, 2024, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Akizungumza na mwandishi wetu, Afisa Elimu Mkoa wa Arusha Mwl. Sara Mlaki amesema kuwa, idadi hiyo ya watahiniwa inajumuisha watahiniwa wa shule (school candidates) na watahiniwa wakujitegemea (private candidates) ambapo watahiniwa 38,594 ni wa shule na watahiniwa 481 ni wakujitengemea.
Amefafanua kuwa, katika idadi ya watahiniwa wa shule 38,594 wavulana ni 18,066 na wasichana 20,528 watakaofanya mitihani, kwenye shule 275 za Serikali na binafsi zikiwa na jumla ya mikondo 1,046.
Aidha, kwa watahiniwa binafsi 481, wavulana ni 199 na wasichana 282, watafanya mitihani yao kwenye vituo 48 vikiwa na mikondo 28.
Hata hivyo, Afisa Elimu huyo, amethibitisha kukamilika kwa maandalizi yote muhimu, ikiwemo semina elekezi kwa wasimamizi wa mitihani hiyo zimefanyika sambamba na usalama wa miundombinu kwa kuzingatia taratibu zote za Mitihani ya Taifa.
Awali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, inawatakia kila la kheri watahiniwa wote katika mitihani hiyo muhimu ya upimaji kwa wanafunzi wa kidato cha pili mwaka 2024.
KILA LA KHERI KIDATO CHA PILI 2024; MWENYENZI MUNGU AWASIMAMIE✍
Post A Comment: