Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeandaa mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wataalamu wa uhifadhi wa mazingira kutoka katika baadhi ya mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ambazo zimeanza utekelezaji wa miradi itokanayo na biashara ya kaboni, ili kuziwezesha kukabiliana na changamoto kubwa ya uelewa iliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Bw. Mtwale amesema hayo leo katika Ukumbi Mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma wakati akifungua mafunzo hayo ya siku mbili kwa maafisa na wataalamu wanaosimamia uhifadhi wa mazingira katika mikoa mitano na halmashauri 19 zinazotekeleza miradi ya biashara ya kaboni nchini.

“Ninawakumbusha lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni, hivyo mada mbalimbali zimeandaliwa kuwawezesha kutambua athari za mabadiliko ya tabianchi na pamoja na kujua njia za kuhimili biashara ya kaboni nchini,” Bw. Mtwale amefafanua.

Bw. Mtawale amesema kuwa, anatarajia mafunzo hayo yatatoa mwelekeo sahihi wa namna bora ya kuratibu na kutekeleza shughuli mbalimbali za kukabiliana na kuongeza uhimili wa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Hakikisheni mnakuwa na ushirikiano wa kutosha katika kuandaa mipango na bajeti ikiwa ni pamoja na kuandaa miradi ya biashara ya kaboni ili kuimarisha ustawi wa taifa letu,” Bw. Mtwale amesisitiza.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo, Afisa Maliasili na Mazingira wa Mkoa wa Manyara Bw. Michael Gwandu amesema kuwa, wamepokea mwongozo na maelekezo mahususi ya namna ya kuzingatia mafunzo ya kukabiliana changamoto ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na biashara ya kaboni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa OR-TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta amesema mafunzo hayo yamehudhuriwa na wawakilishi wa mikoa ya Dodoma, Kagera, Manyara, Arusha, Katavi na Ruvuma pamoja na wa halmashauri 19 ambao katika maeneo yao wameanza utekelezaji wa biashara ya kaboni; Mafunzo yatawajengea uwezo na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa miradi ya biashara ya kaboni pamoja na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeandaa mafunzo hayo ya siku mbili kwa wataalamu wa uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa  jukumu la kusimamia shughuli zote za uhifadhi, utunzaji na usimamizi wa mazingira katika ngazi za mikoa na halmashauri.

Share To:

Post A Comment: