Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema kada ya wataalamu wa maabara kuwa ni chachu ya utekelezaji maono ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha watanzania wanapata huduma fungamanishi za afya kwenye viwango bora.
Waziri Mhagama amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 37 la kisayansi la wataalam wa maabara za Afya nchini na kongamano la 23 la kisayansi laHuqas pamoja na mkutano mkuu wa mwaka unaofanyika Jijini Dodoma Septemba 02, 2024.
Waziri Mhagama amesema ili kutekeleza kwa ufasaha Bima ya afya kwa wote na wananchi kuwa na uhakika wa matibabu lazima kuwa na wataalamu wazuri na wanaowajibika katika eneo la uchunguzi ili kupata majibu sahihi na kwa wakati.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya tunawapongeza wataalamu wa maabara na chama cha wataalamu wa maabara nchini kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuboresha huduma za maabara ya kitaifa na kutambulika kimataifa, kumewezesha maabara 86 nchini kupata vyeti ithibati na kutambulika kimataifa”, ameeleza Waziri Mhagama.
Ameongeza kuwa ithibati hizo ni chachu ya kufanya Tanzania kwenda kasi kwenye eneo la tiba utalii na kuvuna fedha za kigeni kutoka mataifa mbalimbali yatakayo kuja kupata tiba Tanzania.
Hata hivyo amewataka wataalamu hao kutembea kifua mbele kwani serikali chini ya uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan iko pamoja na wataalamu hao kwa kuboresha miundombinu ya huduma za uchunguzi na kutoa ufadhili wa masomo kwa wataalamu wa maabara kupitia Dkt. Samia Scholarship.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laizer amesema, Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kukuza vyama mbalimbali vya kitaaluma ili viweze kusaidia kuishauri Serikali kunako masuala yanayolenga kuimarisha sekta ya afya nchini.
Amebainisha kuwa baada ya Serikali kuwekeza vifaa tiba na miundombinu pamoja na watumishi suala kubwa ni kuhakikisha kuna ubora wa huduma za afya kwani ndio kipaumbele ili mambo yote yaliyofanyika yaweze kuwa na tija kuelekea bima yafya kwa wote.
“ lSuala la usugu wa vimelea vinaweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kama yalivyo magonjwa mengine na ikifika huko maana yake tunaweza kupoteza maisha na gharama kubwa, ieleweke, hakuna huduma bora za tiba bila ya huduma bora za uchunguzi na ndio maana kuanzia mwaka jana Serikali imeanza kutoa ufadhili wa masomi kwa kusomesha wataalamu wa maabara katika ngazi za kati, vyuo vya umma na binafsi ambamba na mashirika ya dini, hii inaonesha dhamira ya Serikali kuendelea kuimarisha sekta hii muhimu”. Amefafanua, Dkt. Laizer.
Post A Comment: