Na. Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF, Mbeya


Wakazi wa Jiji la Mbeya wameipongeza Serikali kwa kuwasogezea elimu ya fedha na huduma mbalimbali za fedha karibu nao.

Wametoa pongezi hizo katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.

Wamesema elimu wanayoendelea kuipata katika maadhimisho hayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wao binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla. 

Bi. Rehema Kassiba wa Kumekucha Saccos ni miongoni mwa wananchi hao, alisema maadhimisho hayo yamewarahisishia upatikanaji wa elimu na huduma za fedha kwa kuwa Serikali imezisogeza huduma muhimu za masuala ya fedha katika maadhimisho hayo.

Aliipongeza Serikali kwa kuandaa maadhimisho hayo na kuahidi atakuwa balozi mzuri kwa kuifikisha elimu aliyoipata kwa wananchi wengine ambao hawajapata nafasi ya kufika viwanjani bua Nzowe yanapofanyika maadhimisho hayo.

“Elimu hii ni nzuri na muhimu kwetu lakini tunaiomba Serikali iandae utaratibu wa kufikisha elimu hii katika maeneo ya vijijini kwa kuwa muda wa maadhimisho haya ni mchache sio rahisi kwa wananchi wote kuhudhuria hususan wale wanaotoka vijijini”, alisema Bi. Kassiba.

Naye Bw. John Mwakipasile, Mjasiriamali wa soko la Mwanjelwa alisema maadhimisho hayo yamewaongezea uelewa wa fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha.

Alisema katika maadhimisho hayo wamepta ujuzi wa matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao, utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni.

Kwa upande wao, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Mbeya, nao wameishikuru Serikali kwa kupeleka Maadhimisho hayo jijini hapo kwa kuwa yamewawezesha kuwapata wananchi wengi ndani ya muda mfupi.

Mratibu wa Mikopo wa Jiji la Mbeya, Bi. Aksa Njidile ni miongoni mwa Maafisa hao,  ambaye aliwakaribisha wananchi kwa kutembela maadhimisho hayo ili wapate elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Alisema wakitembelea katika maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine, watapata elimu ya mikopo mbalimbalimbali inayotolewa na Serikali hususan ile ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

Naye Afisa Vijana wa Jiji la Mbeya, Bi. Ritha Mushi amewahamasisha vijana wa Jiji hilo kutembelea maadhimisho hayo ili watapate elimu ya fursa mbalimbali za kujiinua kiuchumi zinazotolewa na Serikali.

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanatarajia kuongeza idadi ya watu wenye elimu ya fedha na maarifa juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za kifedha pamoja na kuongeza mchango wa Sekta ya Fedha kwenye ukuaji wa uchumi.
Share To:

Post A Comment: