UBALOZI WA China kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wametoa mitungi 800 ya gesi yakiwa na majiko yake kwa walimu, madereva na wahudumu wa Serikali pamoja na Waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha lengo ni kutekeleza sera ya Serikali ya Tanzania pamoja na China katika kutunza mazingira.


Hafla hiyo imefanyika Jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian ,Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Arama ,Mbunge wa Arusha Mjini pamoja na viongozi wa dini

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kugawa mitungi kwa makundi hayo Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema kuwa wanatambua uhusiano mzuri wa kidiplomasia katı ya nchi hizo lakini pia wanafahamu dhamira ya Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kutunza mazingira

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Balozi wa China Mingjian amesema Serikali ya China inaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na uoto wa asili.

Amesema Tanzania ni nchi rafiki wa mazingira na inazingatia uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwamba kwa muda wa miaka mitatu amefanya kazi hapa nchini na anashuhudia juhudi za ajabu ambazo zimefanywa na Tanzania katika nyanja ya utunzaji wa mazingira.

Amesema licha ya Mitungi hiyo ya gesi sio tu itaboresha maisha ya walimu bali pia itapanda mbegu za ulinzi wa mazingira katika mioyo ya wanafunzi na kufafanua Rais Xi Jinping wa China mara nyingi husema maji ya bahari na milima mirefu ni mali ya thamani sana.

"Kama nchi zinazoendelea zinazowajibika, China na Tanzania zote zimekataa kukubali na kukataa kufuata njia ya zamani ya uchafuzi wa mazingira.Badala yake, tumechagua njia mpya ya kipaumbele cha kiikolojia na maendeleo ya kijani...

"Huku tukiendeleza kwa nguvu mazingira, kwa njia ya uchumi na kuboresha maisha ya watu, pia tumechukua jukumu muhimu la kulinda mazingira. Mei mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alipendekeza mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao unadhihirisha kikamilifu falsafa ya Serikali ya Tanzania ya kujali wananchi wake kwanza na kuishi kwa usawa kati ya mwanadamu na maliasili.

"China na Tanzania ni kaka na dada wazuri sana, na pia ni washirika wazuri sana. Daima tunasaidiana. Mwezi uliopita, Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika lilifanya mkutano huko mjini Beijing. Wakuu wa nchi, serikali na wajumbe kutoka nchi 53 akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan walikusanyika Beijing kushiriki, nami nilifuatana na ujumbe wa Rais katika tukio hilo muhimu."

Ameongeza Rais Xi Jinping alitoa hotuba muhimu, na Rais Samia Suluhu Hassan, naye aliiwakilisha Afrika Mashariki, alitoa hotuba kwenye hafla ya ufunguzi.Wakati huo huo, alitangaza hatua za ushirikiano kati ya China na Afrika, katika Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijani, zilipendekeza kuwa China inapenda kutekeleza miradi 30 ya nishati safi katika bara la Afrika ili kuzisaidia nchi za Afrika kufikia maendeleo ya kijani kibichi.

“Ubalozi wa China nchini Tanzania uliunga mkono kikamilifu Mpango wa Nishati safi ya kupikia, na kutekelezwa na Taasisi ya ALAMA kwa msaada mkubwa, kama vile ORYX.Sio tu kwamba ni hatua ya kiutendaji kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Kijani wa China na Tanzania, bali pia ni taswira ya kweli ya urafiki kati ya watu hao wawili.

“Mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili.Katika miaka 60 iliyopita, uhusiano kati ya China na Tanzania umekuwa ukikua na kukua.

“Rais daima amekuwa mstari wa mbele katika ushirikiano kati ya China na Afrika na urafiki wa jadi unaopitishwa kutoka kizazi hadi kizazi na ushirikiano wa pande zote wa sekta mbalimbali na wenye manufaa kwa pande zote unaimarishwa na kuendelezwa.”

Balozi Mingjian amesema kwamba sera ya China nayo imejikita katika kutunza ukijani, hivyo watashiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo hayo na kusisitiza nchi ya China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali ikiwemo ya nishati safi ya kupikia.“China itaendelea kusapoti nishati safi ya kupikia na miradi mingine mingi ya maendeleo itakayoendelea Tanzania,” amesema balozi Mingjian.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Ltd Benoit Araman kuanzia Julai 2021, upatikanaji wa suluhisho la kupika imekuwa mada ya umuhimu mkubwa, chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na leo wako pamoja kuunga mkono utekelezaji wa Programu ya Kupika kwa Nishati Safi nchini Tanzania.

Amesema programu ya nishati safi ya kupikia itachukua miaka 10 kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi kwa ajili ya kupikia kwa angalau asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034. Hivyo kuna haja ya kuungana kufanikisha juhudi hizo.

“Ukizungumza kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wanafunzi wenu na katika mikutano na wazazi itachangia kwa kiasi kikubwa kueneza kwa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania. Ninyi kuwa watumiaji wa Oryx Gas itasaidia idadi ya watu kuona manufaa ya kupika kwa kutumia LPG na kuipitisha zaidi.

“Naushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania, kwa ushirikiano wao, ambao umeruhusu makabidhiano ya mitungi ya gesi na majiko yake 800. Kwa kushirikiana na Gambo Foundation “Alama Africa” na Oryx Gas Tanzania, nchi ya China inaonyesha nia na dhamira yake ya kuunga mkono utekelezaji wa programu ya Kupika kwa Nishati Safi nchini Tanzania.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina faida za kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo ya Uboreshaji wa Afya kwani nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanakufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na chembechembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na Oryx LPG kutaondoa changamoto ya Vifo hivyo.

Hata hivyo amesema Kampuni ya Oryx Gas inafanya kazi kwa bidii kila siku kutekeleza maono ya Rais ya kwamba asilimia 80 ya Tanzania ipate nishati safi ifikapo mwaka 2034. Mpango wa leo na Alama Africa Foundation na Ubalozi wa China nchini Tanzania unachangia katika lengo hilo kubwa kwa kukabidhi mitungi ya gesi na majiko yake 800. Lazima wafanye zaidi.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema Oryx Gas imekuwa Kampuni ya kwanza kwa Arusha kuonesha wamedhamiria kuunga mkono kampeni ya Rais Samia na wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo.

Amesema hata katika utoaji wa mitungi ya gesi 5000 kwa walimu , Oryx Gas walikubali kutoa mitungi na majiko na leo wameendelea kutoa mitungi ya gesi na majiko yake 800 kwa kushirikiana na Ubalozi wa China pamoja na Alama Africa.

“ Tumetoa mitungi na majiko haya ya gesi kutoka kampuni ya Orxy kwa sababu inapatikana kwa urahisi, sio tunawapa mitungi hapa alafu mkashindwa kuijaza…pia bei ya kuijaza ni nafuu naamini wote mnaweza kumudi,” amesema Gambo.

Pia amesisitiza anatambua kazi inayofanywa na Rais Samia katika kuhamasisha nishati lakini pia ni jukumu la wadau mbalimbali kuunga mkono kampeni ya Rais Kama ambavyo wanafanya Oryx Gas na Ubalozi wa China.

Wakati huo huo Sheikh wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA) Mkoa wa Arusha Sheikh Shaban Juma Abdallah amesema jamii inapaswa kuhakikisha na kusimamia vizuri misitu yetu na jambo ambalo Rais amealinzisha la nishati safi ya kupikia anastahili pongezi kwani ni Jambo lenye kujenga huruma kwa kizazi cha sasa na baadae.

Kwa upande wake Mchungaji Julius Talakwa Laiza aliyemwakilisha Baba Askofu wa KKKT Dayosisi Kaskazini Kati Dk.Godson Abel Mollel , amesema elimu hiyo ya nishati safi wataendelea kuitoa
Kanisani kwa kuanza na watumishi wa Mungu wenyewe kwa kuhimizana katika vyao na waumini wao Kanisani watawahimiza kwamba wakitumia gesi watakuwa wameokoa mazingira.

Amesema kuni na mkaa imeharibu misitu yetu lakini wakitumia gesi watakuwa wanafanya mambo matatu muhimu wanahakikisha misitu iko salama, hewa safi na watawaambia ni Kazi waliyoachiwa na Mwenyezi Mungu na kusisitiza mazingira yalitengenezwa na Mungu, hivyo ni vema wakawndelea kutunza mazingira.
















Share To:

Post A Comment: