Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imepokea gari aina ya Toyota Land Cruiser- Pick up kutoka Asasi ya watu na Wanyamapori Tanzania (TPW) kwa ajili ya kukabiliana na Migogoro kati ya Wanyamapori na binadamu katika vijiji vinavyozunguka hifadhi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo leo tarehe 7 Oktoba, 2024 Mkurugenzi wa Miradi Kutoka Asasi ya watu na wanyamapori Tanzania Bw. Charles Trout amesema lengo la Kutoa gari hilo ni kuiwezesha NCAA kuisaidia jamii inayopakana nayo kukabiliana na  Migogoro kati ya binadamu na Wanyamapori wakali hususan Tembo. 

“Asasi ya watu na Wanyamapori Tanzania inasaidia jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi katika kukabiliana na changamoto za  wanyamapori wakali, hivyo tunaamini kuiwezesha NCAA gari hili itaisaidia jamii inayopakana nayo kupata msaada wa haraka zaidi pale wanapokumbana na changamoto za Wanyamapori wakali na waharibifu kuingia kwenye mashamba ya wananchi” alisema Trout 

Baaada ya kukabidhiwa gari hilo Kaimu Kamishina wa Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Gloria Bideberi alisema ujio wa gari hilo litasaidia kuongeza jitihada zinazofanywa na Mamlaka hiyo kukabiliana na migorogoro kati ya wanyamapori na jamii zinazoizunguka Hifadhi hiyo  katika Wilaya za Karatu, Monduli, meatu na Ngorongoro.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Uhifadhi kutoka TPW, Bw. Neovitus Sianga alisema kwamba gari lililokabidhiwa leo ni moja ya nyezo ambazo zinaendelea kutolewa na asasi hiyo kwa lengo la kusaidia jamii hasa zile zinazopaka na Hifadhi kukabiliana na adhari za wanyamapori. 

“Kwa upande wa vijiji vinavyopakana na Ngorongoro,tunatarajia kuwa na vijiji 12 ambapo kwa sasa tumeshaanza kufanya kazi na vijiji 8 ambavyo tumeviwezesha kuanzisha maafisa migogoro wawili kila Kijiji na kuwapatia vitendea kazi kwa ajili ya kukabiliana na wanyamapori hasa tembo” Alisema Neovitus

Asasi TPW imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kuweka kituo cha upatikanaji wa taarifa za haraka kwenye ofisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuwezesha utatuzi wa migogoro kwa haraka zaidi pale taarifa inapoletwa.






Share To:

Post A Comment: