Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendela kufanya kazi na Mfuko wa Watoto wa Umoja na Mataifa (United Nations Children's Fund - UNICEF) kwa kuwa inatambua ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na UNICEF kupitia afua mbalimbali katika Sekta ya Afya.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Oktoba 3, 2024 wakati akimkaribisha Mwakilishi mpya wa shirika hilo la UNICEF nchini Tanzania Bi. Elke Wisch katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam.
"Tutaendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Kuboresha huduma za Afya ya Msingi (PHC) kupitia kuimarisha uwezo wa jamii na familia ikiwa ni pamoja na kutafuta huduma sahihi za malezi kwa watoto wadogo ili kuhakikisha wanakua kwa njia bora ifikapo mwaka 2027." Amesema Waziri Mhagama
Vilevile, Eneo jingine ambalo Tanzania na UNICEF wanayoshirikiana ni katika kukuza huduma za afya kupitia Wafanyakazi wa huduma za afya katika jamii na vituo vya afya ambao wanatoa huduma za PHC zenye ubora, ufanisi, usalama, na heshima.
Wizara imeweza kujumuisha wafanyakazi wa Maendeleo ya Watoto Wadogo (ECD) katika mwongozo wa Kitaifa ukiwemo mwongozo wa Kitaifa wa huduma za watoto wachanga, Usimamizi wa mchanganyiko wa magonjwa ya watoto (IMCI), Nyenzo za ufuatiliaji wa ukuaji ambazo zinajumuisha vitabu vya afya vya watoto kwa wavulana na wasichana.
"Kifurushi hiki kinakusudia kutoa maarifa na ujuzi kwa wafanyakazi wa afya ili waweze kutoa huduma na ushauri kuhusu maeneo ya ECD kwa wanawake wajawazito, wazazi, na walezi wanaotembelea vituo vya afya." Amesema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Bi. Elke Wisch amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika Sekta ya Afya kwenye mikoa zaidi ya 10 nchini Tanzania, ambapo UNICEF inapatikana ili kutekeleza na kufikia upatikanaji wa jumla na matumizi ya huduma za maji safi na usafi katika vituo vya afya ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
"Tupo hapa kwa kufanya kazi na wewe (Waziri wa Afya) kwa kushirikiana na timu yako, tutafanya kazi pamoja katika kuzuia magonjwa ya milipuko ikiwemo ya Kipindipindu, Mpox na magonjwa mengine, tutaendelea kushirikiana katika vipaumbeke vyetu ili kuwaepusha Watanzania na magonjwa." Amesema Bi. Elke Wisch
Post A Comment: