SERIKALI imesema kuwa ipo imara daima katika dhamira yake ya kujenga mazingira rafiki ya biashara kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kadhalika imesema kuwa imetekeleza Sera na Mipango mbalimbali ili kukuza uchumi na kupunguza utegemezi kwenye bidhaa.
Hayo yamesemwa Leo Octoba 9, 2024 na Naibu Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati akizindua benki ya Access jijini Dar es salaam.
"Tunapokusanyika hapa leo, uchumi wa Tanzania unaendelea kuonyesha ustahimilivu na ukuaji thabiti. Uchumi wa taifa letu umeendelea kukua, ikichangiwa hasa na sekta ya kilimo, madini, utalii,ujenzi na sekta ya fedha.
Jitihada hizi zimetoa matokeo chanya, kama inavyothibitishwa na mchango unaoongezeka wa utengenezaji, huduma, na teknolojia kwa Pato la Taifa" amesema Mhandisi Mahundi
Amesema eneo la kimkakati la Tanzania lina rasilimali nyingi zinazoifanya nchi kuwa eneo lenye nguvu ya kiuchumi kikanda.
"Tunakuza kikamilifu utangamano wa kikanda na biashara huria ili kuongeza ushindani wa kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa kigeni,
"Kuingia kwa Access Bank nchini Tanzania kunaenda sambamba na dira ya serikali yetu ya kuwa taifa lenye ustawi na jumuishi. Dhamira ya benki kutoa huduma za kifedha kwa gharama nafuu ni suala muhimu katika kusaidia ukuaji na maendeleo ya uchumi"amesema Mahundi
Mhandisi Mahundi amesema Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha sera zinazolenga kukuza uchumi, kutengeneza ajira na kuleta maendeleo kwa kijamii.
Post A Comment: