Na : Jusline Marco;Arusha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka huu upatikanaji wa dawa umefikia wastani wa asilimia 85 zinazohitajika kwenye maeneo yote ya utoaji huduma huku kwa upande wa zahanati upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 76.
Akifungua Kongamano la Bima ya Afya kwa wote na Jukwaa la Kitaifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya linalofanyika jijini Arusha, Warizi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa amesema pamoja na mapungufu yaliyopo bado serikali inajitahidi ili kuweza kuyafikia malengo.
Mhe.Majaliwa ameiagiza wizara ya afya nchini kuweka utaratibu na mkakati wa namna ya kuufikia umma na kuuelimisha umuhimu wa Bima ya Afya na faida yake kwa kurudi katika mfumo wa zamani wa kuweka magari yenye sinema zinazotoa elimu ya afya kwa wananchi.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama mesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiipa gharama kubwa serikali ya kutumia fedha nyingi kutibu wananchi na kununua vifaa tiba ili kuweza kuwaokoa ambapo katika kipindi cha miaka 3 sekta ya Afya imepokea zaidi ya shilingi trilioni 6.2 kwa ajili ya kushughulikia mambo mbalimbali ya kimsingi ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya sekta ya afya.
Awali akizungumza katika Kongamano hilo kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara ya Afya, Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Tumain Nagu amesema kongamano hilo ambalo limekutanisha wadau mbalimbali ikiwemo wizara na taasisi za serikali ya Tanzania na Zanzibar kuweza kutoa fursa za kubadilishana uwezo utakaowezesha utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote na kuwezesha ugharamiaji endelevu wa hudumaza afya.
Vilevile amesema katika kongamano hilo wataweza kuandaa mikakati itakayojumisha wadau wote katika kutekeleza sheria ya bima ya afya kwa wote ambapo malengo ya kongamano hilo ni kuimarisha ushirikiano wa kisekta katika kugharamia huduma za afya,kuimarisha uwezo wa watekelezaji wa bima ya afya kwa wote katika kuwajengea uwezo wataalam wa afya,wasimamizi na waendeshaji skimu za bima ya afya ili kusimamia utekelezaji wa bima hiyo kwa ufanisi pamoja na kuimarisha wajibikaji,uwazi na matumizi ya tehama katika kuishirikisha jamii kwenye masuala ya utekelezaji wa sheria ya bima ya afya.
Ameongeza kuwa jitihada za wadau mbalimbali wa afya katika kushirikiana na serikali kuwapatia wananchi huduma bora za afya zinaleta mafanikio hasa katika afya ya msingi ambapo ni matumaini ya wizara kuendelea na ushirikiano huo ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana nchini kwa watu wote kupitia mpango mkakati wa tano wa sekta ya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Salim Slim amesema licha ya mafanikio ambayo Wizara ya afya Zanzibar imekuwa ikiyapata,Wizara hiyo kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa wataalam katika eneo la huduma za afya ,kuwepo kwa wachangiaji wachache katika mfuko wa fedha pamoja na uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya kujiunga na huduma ya afya.
Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia masuala ya Afya na Ukimwi Jackline Kahinja akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameiomba serikali kuiwezesha Bohari ya Dawa Tanzania fedha za kutosha ili iweze kujisimamia katika uzalishaji na usambazaji wa dawa kwa wananchi.
Amesema kama kamati itaendelea kusisitiza utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote iliyopitishwa na Bunge la Tanzania mwezi Novemba 2023,kuhakikisha wanafuatilia kwa kina vyanzo vya mapato vya ndani kwaajili ya kundi la watu wasiojiweza.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Denis Londo akizungumza katika Kongamano hilo amesema kuwa nchi wanachama zinaendelea kushirikiana katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo muhimu ikiwemo mifumo na sera za afya,kudhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, usalama wa dawa na chakula pamoja na afya ya mama,mtoto na lishe.
Amesema kupitia utekelezaji wa itifaki wa soko la pamoja ambayo ni hatua ya pili ya mtangamano wa kikanda,nchi wanachama imehakikisha kuwa huduma za afya zinapatikana kwa urahisi na zenye viwango vya ubora vinavyokubalika ambapo soko la pamoja linawezesha uhuru wa watu,bidhaa na huduma kuvuka mipaka mbali na nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki hali inayochangia kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za afya na kuboresha ustawi wa jamii nzima ya jumuiya ya Afrika Mashariki.
Post A Comment: