Na. Farida Ramadhani na Joseph Mahumi, WF, Mbeya
Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 133.310 kwenye sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kuwawezesha mitaji, kutoa mafunzo ya ujasiriamali, matumizi ya huduma za fedha, tafiti kuhusu sekta ya fedha na kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye sekta ya fedha.
Hayo yameelezwa jijini Mbeya na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yenye kaulimbiu “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi” kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, yanayofanyika katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.
Alisema Serikali imepanga kutekeleza hayo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/22 -2025/26 ambapo wahusuka wakuu ni Taasisi za Fedha na watoa huduma za Fedha.
”Watoa huduma za Fedha watekeleze majukumu yao kulingana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa 2021/22-2025/26, Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2021/22-2029/2030 na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano (5) wa Elimu ya Fedha (2019/20-2025/26) kwa Maendeleo ya Sekta ya Fedha na Nchi kwa ujumla” aliagiza Prof. Mkenda.
Alisema Serikali imekuwa ikiboresha Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Fedha kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Mhe. Prof. Mkenda alisema katika jitihada hizo Serikali imefanikiwa kuongeza mchango wa Sekta ya Fedha katika ukuaji wa uchumi pamoja na kuongeza upatikanaji na utumiaji wa huduma jumuishi za fedha kutoka asilimia 65 mwaka 2019 hadi asilimia 76 mwaka 2023.
Aidha, alitaja mafanikio mengine kuwa ni watoa huduma Ndogo za Fedha kutambuliwa, kusajiliwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania, kuongezeka kwa upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo na wa kati pamoja na kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha wananchi kutumia huduma rasmi za fedha, ambapo jumla ya Mikoa 12 na Halmashauri 65 na wananchi zaidi ya 32,000 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Mei, 2024 hadi Septemba, 2024 walifikiwa.
Aidha, alisema mtaala mpya wa elimu umejumuisha elimu kuhusu fedha kwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne ambapo utekelezaji wake masomo yanahusu masuala ya fedha na ujasiriamali yatakua ya lazima.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja alizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema Sekta ya Fedha ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Alisema Sekta hiyo, pamoja na mambo mengine ina majukumu mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa za masoko, kuhamasisha kuweka akiba na kuwezesha kuuza na kununua bidhaa, uwekezaji na mitaji, kuwezesha biashara, kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia vihatarishi katika sekta ya fedha, kujipanga na maisha ya uzeeni pamoja na kuelimishwa umma kuhusu masuala ya bima.
Dkt. Mwamwaja alisema kuwa Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa itafanyika kwa umahiri mkubwa na anatarajia kuea mwisho wa madhimisho hayo yatawezesha malengo ya Wiki hiyo yatafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Post A Comment: