Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha wawekezaji katika maeneo yenye nishati jadidifu ili kuyaendeleza na hivyo kuwezesha azma ya nchi kuwa na umeme unaotokana na vyanzo mchanganyiko.
Amesema hayo jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ikiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya Nishati Jadidifu inayotokana na Jotoardhi, Upepo na Jua kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
"Tumeshayatambua maeneo ambayo nishati jadidifu inapatikana, kwa upande wa Jotoardhi tunaendelea na uhakiki wa rasilimali hiyo ambayo inahusisha uchorongaji wa visima." Amesema Dkt. Mataragio
Dkt.Mataragio amesema Nishati Jadidifu kama Jotoardhi, Jua na Upepo ni miongoni mwa nishati safi ambazo zinaendana na malengo ya dunia ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga alisema rasilimali ya Jotoardhi ni jadidifu na endelevu na inatumika kwa kuzalisha umeme na matumizi mengine.
“Tanzania inakadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa jotoardhi usiopungua megawati 5,000 kutoka katika vyanzo 52 vinavyopatikana ndani ya mikoa 16 nchini." Alisema Mhandisi Nyamo-Hanga
Akielezea hatua za utekelezaji wa miradi hiyo Mhandisi Nyamo-Hanga alisema mradi wa Ngozi uliopo mkoani Mbeya upo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali jotoardhi ambayo inahusisha uchorongaji wa visima vya uhakiki.
Alisema Mradi huo ukikamilika utazalisha megawati 70 ambapo utaanza na megawati 30.
Mradi mwingine ni Kiejo-Mbaka ambao upo wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya ambao umefikia hatua ya uhakiki wa rasilimali ya joto ardhi ikihusisha uchorongaji wa visima virefu vya utafiti.
Alisema mradi huo utazalisha Megawati 60 ambapo utaanza na megawati 10.
Aliongeza kuwa, Mradi wa Songwe upo katika hatua ya uchorongaji wa visima vinne vya uhakiki wa rasilimali.
Akieleza kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme jua, Mhandisi Nyamo-Hanga alisema utafiti unaonesha maeneo mengi nchini yanaweza kufungwa mitambo ya umeme jua ikiwemo Dodoma, Singida, Tabora, Arusha, Shinyanga na Iringa.
Alisema mradi wa umeme jua ambao upo katika hatua ya utekelezaji ni wa megawati 150 uliopo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambao unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itazalisha megawati 50 na awamu ya pili megawati 100.
Alisema miradi ya upepo ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu na itakapokamilika itaongeza kiwango cha umeme kinachotokana na na nishati jadidifu.
Post A Comment: