Mkurugenzi wa Idara Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais - TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amezihimiza timu za usimamizi wa shughuli za Afya ngazi ya Halmashauri (CHMT) na mkoa (RHMT) nchini kuwa na utaratibu wa kufanya vikao vya kila mwezi kupitia takwimu za utoaji wa huduma za Chanjo ili kubaini mapungufu na kuchukua hatua stahiki.

Dkt. Mfaume ametoa rai hiyo mkoani Tabora wakati wa kikao cha majumuisho ya ziara ya usimamizi shirikishi na ufuatiliaji wa huduma za Chanjo na mikakati ya kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika Mikoa ya Katavi na Tabora.

Dkt. Mfaume amesema Tabora na Katavi ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa na kiwango kisichoridhisha cha utoaji wa huduma za chanjo, hali inayochangia baadhi ya walengwa wa chanjo kutofikiwa, na kuwepo kwa hatari ya milipuko wa magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo.

" 'Ume-plan' kufanya 'outreach' 30 kwa robo mwaka unafanya 'outreach' moja unasitisha 29 na hakuna sababu za msingi, Suala hili linachangia kwa kiwango kikubwa baadhi ya walengwa kutofikiwa na huduma za Chanjo, hii haikubaliki''. amesema

Ziara hii mahsusi imekuja kufuatia kutoridhishwa kwa kiwango cha huduma za Chanjo katika Mikoa hiyo sambamba na kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kuaharisha na kutapika lakini pia kuangalia maandalizi ya Mikoa hiyo kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza.

Akisisitiza hilo Dkt. Mfaume amesisitiza waratibu wa chanjo na CHMT kuwajibika na kuacha kutafuta utetezi na sababu zisizo na mashiko zinazochangia hali isiyoridhisha ya utoaji wa chanjo kwa wananchi. Aidha amewaomba wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanakamilisha ratiba za Chanjo ili kuwakinga dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Kwaupande wake Bi.Joseline Ishengoma Mratibu wa huduma za chanjo kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI amesema vituo vingi ambayo vimefanyiwa usimamizi havitoi huduma za chanjo ipasavyo hali inayoweza kupelekea kushuka kwa kinga jamii dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa Chanjo na kusababisha hatari ya milipuko ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, hivyo amewasihi wasimamizi ngazi ya Halmashauri na Mikoa kuongeza juhudi katika kusimamia huduma hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) Ofisi ya Tanzania, Dkt. William Mwengee amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha huduma za Chanjo zinatolewa kwa ufanisi Nchini.

Ziara hiyo ya usimamizi shirikishi na ufuatiliaji imehusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI wakiongozwa na mkurugenzi Dkt. Rashid Mfaume kwa kushirikiana na Timu za usimamizi wa shughuli za Afya za Mikoa na Halmashauri, wadau wa maendeleo ambao ni shirika la Afya ulimwenguni (WHO) na Shirika la Jhpiego kupitia mradi wa USAID Afya yangu Mama na Mtoto.







Share To:

Post A Comment: