Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amefanya ziara ya kikazi mkoani Njombe mnamo Oktoba 10, 2024, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiuwekezaji kati ya Tanzania na China.

Alipokelewa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ambaye alitoa shukrani kwa serikali ya China na wawekezaji wake kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya mkoa huo. 

Mhe. Mtaka alisisitiza kuwa Njombe ina fursa nyingi, hasa katika sekta za kilimo, viwanda, na uvuvi, zinazoweza kuwanufaisha wawekezaji wa Kichina na kukuza uchumi wa mkoa wa Njombe.

Balozi Chen alizindua kliniki ya madaktari bingwa kutoka China, kliniki ambayo inalenga kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Njombe. Katika hotuba yake, Balozi Chen alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huu, akisema, “China ina nia ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, hususan kwenye sekta za afya, miundombinu, na viwanda, ili kuhakikisha kuwa urafiki wetu unaleta manufaa kwa pande zote mbili.”

Akiendelea na ziara yake, Balozi Chen alitembelea eneo la ujenzi wa kiwanda cha nondo kinachomilikiwa na wawekezaji wa China, ambapo alikagua maendeleo ya mradi huo. Alieleza kuwa uwekezaji kama huu ni muhimu kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Pia, alitembelea Stesheni ya TAZARA Makambako.

Mhe. Anthony Mtaka alimkaribisha Balozi Chen kutembelea mkoa wa Njombe tena, huku akielezea kuwa mkoa huo una fursa nyingi zinazoweza kuendelezwa kwa ushirikiano na China. Akisisitiza umuhimu wa uwekezaji, alisema, “Mkoa wa Njombe uko tayari kupokea wawekezaji kutoka China, na tunawaalika kuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali .”

Ziara hii ya Balozi Chen imeimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China, huku pande zote mbili zikihakikisha kwamba uwekezaji unaleta manufaa kwa wananchi wa Njombe na taifa kwa ujumla.












Share To:

Post A Comment: