Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa wananchi wa Tanga kuweka kipaumbele suala la usafi katika maeneo wanayoishi pamoja na upandaji wa miti ikiwa moja ya njia ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira.


Mhe. Dkt. Kijaji amesema kwa kuanza na kila mwanafunzi anatakiwa kuwa na mti wake ambapo atausimamia hadi anapomaliza shule vivyo hivyo kwa wazazi na walezi nao wanatakiwa mfano wa kuigwa kwa Watoto wao katika utunzaji wa mazingira.


Ameyasema hayo Oktoba 24,2024 wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga ambapo aliweza kutembelea, kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo na kufanya mikutano ya kuongea na wananchi mkoani humo.


“Naomba nichukue nafasi hii kuwaeleza kuwa njia sahihi ya kujilinda ni kulinda mazingira yetu kwani tusipofanya hivyo athari zake ni kubwa zaidi kwetu na vizazi vyetu.


“Lazima tutunze mazingira, lazima tupande miti na mikoko ambayo ndio yenye nguvu ya kuzuia mmomonyonyo wa ardhi kwenye kingo ya bahari, hivyo tupunguze shughuli zetu ambazo zinaharibu mazingira,” amesema Mhe. Dkt. Kijaji


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilida Burian amesema mkoa una misitu yenye takriban hekta 735,903 ikiwemo Misitu ya Serikali Kuu, Misitu ya Hifadhi ya Halmashauri, Misitu ya Hifadhi ya Vijiji, Misitu inayomilikiwa na taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi. 


Mkoa pia una mashamba matatu ya miti ya kupandwa ya Serikali Kuu, mashamba hayo ni Shamba la Miti Shume hekta 4863, Shamba la Miti Longuza hekta 7067 na Shamba la Miti la Korogwe Fuel hekta 10,850. 


Mhe. Balozi Dkt. Burian amesema changamoto zinazokabili misitu hiyo ni uchungaji wa mifugo kwenye misitu, moto, kilimo cha kuhamahama, uchomaji wa mkaa ndani ya misitu ya hifadhi na uvunaji usioendelevu.


“Tunaishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwezesha ujenzi wa ukuta Wilaya ya Pangani wenye urefu wa mita 960 lakini nitumie fursa hii kukuomba tena ili tukamilishe eneo lililobaki.”


Ameongeza kuwa Mkoa unaendesha kampeni ya usafi wa mazingira inayojulikana kama Msaragambo, Kupitia kampeni hiyo wananchi wanaelimishwa na kuhamasishwa kuishi katika mazingira safi wakati wote na pia kushiriki kwa pamoja kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika kufanya usafi kwenye maeneo korofi. Kampeni hii imeleta mafanikio kwa kupunguza uchafu katika maeneo mengi na korofi. 


Ikumbukwe, halmashauri ya Jiji la Tanga ilishika nafasi ya kwanza Kitaifa kwa usafi wa mazingira mwaka 2023.







Share To:

Post A Comment: