Na OR - TAMISEMI, Tabora


Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt Emmanuel Shindika amesema Programu za Elimu ya Watu Wazima zitasaidia  kuinua uchumi na elimu ya Mtanzania kutokana na uwekezaji na maboresho yaliyofanywa na Serikali na Wadau.

Dkt. Shindika akimwakilisha Mhe. Dkt. Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania na Waziri wa Nishati aliyasema hayo wakati akifunga wiki ya Elimu ya Watu wazima iliyofanyika Kitaifa mkoani Tabora na kufikia kilele siku ya ijumaa tarehe 11 Oktoba, 2024 katika viwanja vya Chipukizi vilivyopo katika Manispaa ya Tabora.

“Serikali imefanikiwa kuwarejesha vijana waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa elimu ambapo vijana 12,000 wamenufaika na mafunzo ya muda mrefu na vijana zaidi ya 30,000 wakinufaika na mafunzo ya muda mfupi yanayolenga kuwandaa kuwa na ujuzi wa kiufundi na biashara ambao unawasaidia kuanzisha miradi ya kiuchumi inayochangia kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa hii inasaidia kuwapa fursa wale waliokatishwa masomo yao au waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu kupitia mfumo rasmi, hivyo kuwapa nafasi ya kujikomboa kielimu na kiuchumi” alisema Dkt. Shindika.

Alisema Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kukishirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wanatekeleza Mradi wa Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi ambapo katika mwaka wa masomo 2024 wanafunzi wapatao 18,886 wameweza kudahiliwa na elimu hii inatolewa kupitia vituo vya shule huria (Open Schools) vipatavyo 763. Pia Programu za mafunzo ya ujasiriamali, ufundi na teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) zimewawezesha vijana na watu wazima waliokuwa nje ya Mfumo Rasmi wa elimu kujipatia ujuzi wa kiteknolojia unaowezesha kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali za viwanda, kilimo na biashara. 

Kwa upande wake Abdul M. Maulid, Kaimu Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia alisema maadhimisho hayo yanafanyika kila mwaka katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya na  yana umuhimu wa kuhakikisha elimu inawafikia watu wote na ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha watu wazima kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi hasa wakati huu ambapo yanatokea mabadiliko makubwa ya Kisayansi na Kiteknolojia Duniani.

Akitoa salamu za awali Upendo Rweyemayu Afisa Elimu Mkoa wa Tabora alitoa rai kwa wanatabora kuhakikisha wanawaandikisha watoto wao kuingia darasa la kwanza mwaka 2025 pamoja na kuwahimiza wanafunzi watoro sawa na asilimia 40 ambao hawafiki shuleni ili kupunguza tatizo la watu wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu miaka ya mbele.

Naye Ayoub Kafyulilo Mratibu wa masuala ya Elimu UNICEF Tanzania alisema kwa Tanzania wanatekeleza Mradi wa Elimisha Mtoto unaolenga kuhakikisha Watoto wote waliokosa elimu katika mfumo rasmi wanapatiwa elimu, na Mradi wa Elimisha Mtoto wa kike kuwawezesha watoto wa kike kufikia ndoto zao. 

Juma la Elimu ya Watu Wazima limefikia kilelel tarehe 11 Oktoba, 2024 na wananchi wa Tabora walijitokeza kujifunza kuhusu Programu zake na baadhi ya Wadau wanaofadhili afua mbalimbali za Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi walihudhuria ambao ni UNICEF, UNESCO, CARE International, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na DVV International huku kauli mbiu ya mwaka 2024 ni ‘Ujumuishi katika Elimu bila Ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo’

Share To:

Post A Comment: