Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeanzisha kitengo maalum kwa wagonjwa wa kiharusi ili kuhakikisha wagonjwa wa kiharusi wanapata huduma stahiki kwa haraka ikiwa ni mkakati wa kuendelea kupunguza vifo na madhara ya muda mrefu yatokanayo na ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji MNH Prof. Mohamed Janabi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu kuboreshwa na kuimarika kwa kliniki za magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu ikiwa ni miaka miwili tangu kliniki hizo zilipohamishiwa Muhimbili Mloganzila Oktoba, 2022.
Prof. Janabi amebainisha kuwa kitengo maalum cha kiharusi kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 10 kwa wakati mmoja na kina mashine maalum za ufuatiliaji wa mienendo ya mgonjwa kadiri anavyopatiwa matibabu ili kumuwezesha mtaalam kuchukua hatua stahiki kutokana na changamoto aliyonayo mgonjwa.
Aidha ameongeza kuwa kitengo cha ubongo na mishipa ya fahamu kimeshuhudia ongezeko la wagonjwa wa nje kutoka wastani wa wagonjwa 50 mwaka 2022 na kufikia wagonjwa 150 kwa siku ambapo katika kila wagonjwa 10, wagonjwa 6 wana kiharusi.
“Katika kukabiliana na magonjwa ya ubongo na mishipa ya fahamu tunawahudumia wagonjwa kwa kutumia wataalam bobezi wa magonjwa wa fani mbalimbali ikiwemo wa magonjwa ya dharura, radiolojia, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, ICU na fiziotherapia” amebainisha Prof. Janabi.
Prof. Janabi amesema kuwa kitengo hicho kinatoa dawa maalum kwa magonjwa ya kutetemeka na kushindwa kutumia viungo vya mwili (Movement Disorder) kama vile mikono, miguu na shingo (Dystonia) na kutoa huduma za matibabu ya kifafa kwa watu wazima ambapo kwa kipindi cha miaka miwili wamehudumia wagonjwa 338 wa nje na wa ndani 4,850.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fhamu Dkt. Mohamed Mnacho ameishauri Jamii kuepuka unywaji wa pombe uliopitiliza kwa kwa kuwa kunaweza kuathiri seli za ubongo wa binadamu ambapo kunaweza kusababisha kiharusi.
Post A Comment: