Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi. Victoria Kwakwa, amesafiri kwa njia ya Treni ya Kisasa-SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 3 nchini Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia. Katika ziara hiyo, anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kuhusu ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na uwezekano wa Benki hiyo kushiriki katika ufadhili wa vipande vya SGR vilivyosalia.
Bi Kwakwa alitumia fursa hiyo kuipongeza Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa mradi huo wa SGR ambao amesema utakuwa kichocheo kikubwa cha usafirishaji wa abiria na mizigo na kuchangia ukuaji wa uchumi si tu kwa Tanzania bali kwa nchi zote za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Katika safari hiyo Bi. Kwakwa aliambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bw. Nathan Belete, na Maafisa Waandamizi wa Benki hiyo Bw. Nicholas Soikan na Bi. Makiko Watanabe.
Post A Comment: