Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewataka Viongozi wa kidini na kimila kushirikiana na Watendaji katika sekta ya Elimu kudhibiti suala la maadili kwa watoto.
Mhe. Mpango ametoa rai hiyo Oktoba 09, 2024 mkoani Tabora akizungumza na Wananchi wa mkoa huo, ambapo amesisitiza viongozi na jamii kwa ujumla kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa Watoto.
‘’Wapo watu wa hovyo ambao wanatuharibia Watoto, tunafikiri wamekwenda shule kumbe wanawafundisha mambo ya hovyo. Wazazi msitelekeze Watoto, kagueni wanayojifunza Shuleni hii itasaidia kudhibiti vitendo visivyofaa vya kimaadili’’ alisema Mhe. Mpango.
Aidha Dkt. Mpango amesema Serikali inatambua Haki ya kila mtoto kupata Elimu ndio maana inatoa elimu bila ada kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita, hivyo amewasisitiza Wazazi kupelekwa watoto wenye umri wa kwenda Shule kusoma.
"Tunafahamu kuna changamoto ya watumishi hususan walimu, na baadhi ya shule zina walimu wachache sana, nimeielekeza ofisi ya Rais TAMISEMI katika mgao ujao wa watumishi watoe kipaumbele kwa wilaya ya Uyui na kuutazama mkoa huo kwa jicho la pekee" Alisema Mhe. Mpango
Sambamba na hilo Dkt. Mpango ameitaka Ofisi hiyo kuanza mchakato wa kuongeza nyumba za watumishi katika sehemu mbalimbali.
Post A Comment: