Imeelezwa kuwa Kampuni za Kitanzania zinaendelea kuwa vinara wa kutoa huduma na bidhaa za migodini kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kuwa chachu ya watanzania kuwekeza katika Sekta ya Madini nchini kupitia Sheria ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content) ambapo Jiji la Mwanza limekuwa mfano mzuri kupitia Kampuni za JC Gear Group (T) Limited na Rock Solutions Limited, kampuni za ndani zinazojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa vifaa na bidhaa muhimu zinazotumika katika shughuli za uchimbaji migodini.
Hayo yamebainishwa Septemba 30, 2024, jijini Mwanza na Viongozi wa Kampuni hizo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini kuhusu maendeleo ya Miradi ya Kampuni hizo mbili tofauti zilizojikita jijini Mwanza kwa asilimia kubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya JC Gear Group (T) Limited, James Makanyaga alisema kuwa, Kampuni hiyo imejikita katika kutengeneza bidhaa muhimu zinazotumika katika mitambo ambayo hutumika migodini pamoja mashine za viwandani, magari ya usafirishaji, na vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na matengenezo na ukarabati wa mashine, usambazaji wa vipuri kama bearings, shafts, na gearboxes, pamoja na utoaji wa ushauri wa kiufundi kwa wateja wao.
Makanyaga maarufu kama Jimmy alisema kupitia uwekezaji huo, wanajivunia kutoa ajira za moja kwa moja 36 kwa vijana ambao wote ni watanzania, kwani kupitia kiwanda hicho vijana wamepata mafunzo kuhusu teknolojia mpya na ya kisasa na kwamba matarajio yao ni kuongeza nafasi za ajira kadiri watavyokuwa wanapata kazi kutoka kwenye migodi.
“Sisi bidhaa zetu hazibagui, zinatumika kwenye migodi yote, na katika mitambo yote hadi chini kabisa kwenye migodi, kwa mfano tunakarabati na kutengeneza bidhaa kulingana na mahitaji ya mteja wetu, tunakarabati na kutengeneza bidhaa ambazo hutumika sana kwenye mashine za uchimbaji madini, vifaa vya kuvuta na kusaga mawe, na mitambo mizito inayotumika kwenye uchimbaji wa chini ya ardhi au juu ya ardhi, pia, mitambo inayozalisha umeme, kama vile turbines, hutumia gia kwa ajili ya kusambaza nishati, sisi tunatengeneza hizo hapa” alisisitiza Makanyaga.
Aliongeza kuwa, kama kampuni ya ndani inayotoa huduma za ubunifu na ufundi wa hali ya juu, JC Gear Group (T) Limited ni mfano mzuri wa jinsi Watanzania wanavyoweza kuwekeza katika sekta ya mitambo na kuleta tija kwenye sekta ya madini na viwanda vingine vinavyohusiana kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Rock Solutions Limited Fabian Mayenga alieleza kuwa Kampuni hiyo imejikita katika usambazaji wa vifaa vya uchimbaji madini kuanzia juu hadi chini ya migodi.
“Kampuni yetu itatoa vifaa vya msingi vinavyohitajika kwa ajili ya uchimbaji wa madini, kama vile nyundo zinazotumika kwenye uchimbaji, compressors, na vilainishi vya mitambo, huduma zetu ni za kina na zinagusa kila nyanja ya uchimbaji wa madini, kutoka usambazaji wa vifaa vya kisasa kama huduma za kiufundi kama msaada wa ufungaji wa vifaa, matengenezo, na ushauri wa kitaalamu” alieleza Mayenga.
Aliongeza kuwa hivi sasa Kampuni ina wafanyakazi 50 wote wakiwa ni Watanzania na kwamba siku za usoni wataongezeka kufikia hadi 150 kulingana na uzalishaji na kadri biashara itakavyokuwa huku akisisitiza kuwa shughuli rasmi za uzalishaji zinatarajia kuanza mwanzoni mwa mwaka 2025.
Naye, Mkaguzi Mwandamizi wa Hesabu za Migodi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa Mwanza Elinami Kimaro alisema kuwa, lengo Serikali ya Tanzania kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 ni pamoja na kuweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki kikamilifu kwenye sekta ya madini kupitia Kanuni ya Local Content.
“Nitoe wito kwa wenzetu Watanzania waliopo katika nafasi tofauti katika Kampuni zinazomiliki migodi hapa nchini kutoa kipaumbele Watanzania wanaoomba hizo kazi, maana kuna malalamiko tunapokea kuwa wenzetu walioko huko kuna namna wanatukwamisha na kwamba Sheria ya Madini kifungu cha 102 inaelekeza kuwapa kipaumbele wazawa kushiriki katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, iwe kwa kutoa bidhaa, huduma, au ajira” alisisitiza Kimaro
Kampuni kama JC Gear Group (T) Limited na Rock Solutions Limited zinachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha Kanuni hiyo ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa kutoa bidhaa na huduma zinazosaidia kuendeleza sekta ya madini na viwanda vingine nchini.
Kwa kuzingatia michango ya Kampuni hizo katika sekta ya madini, ni wazi kuwa Watanzania wamejipambanua kama wadau muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inapata vifaa na huduma za hali ya juu, zinazosaidia kuboresha ufanisi wa kazi na kuongeza tija kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuonesha kuwa Watanzania wana uwezo wa kutoa huduma bora zinazokidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuleta ushindani wa haki na kuongeza ajira kwa wananchi.
Post A Comment: