Madaktari bingwa wa Rais Samia wamerejesha furaha ya Zaina Mdee (46) mkazi wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro aliyesumbuliwa na tatizo la meno kwa zaidi ya miaka 27 sasa.

Akizungumza mara baada ya kupata huduma za matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari bingwa wa Rais Samia walioweka kambi kwa siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Same, Bi. Mdee amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasogezea huduma za kibingwa katika maeneo yao na kufanya wasisafiri umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufuata huduma hizo.

 “Nimekuja hapa hospitali ya Wilaya ya Same kupata huduma ya matibabu nilikuwa na tatizo la meno yamenisumbua kwa muda mrefu tangu nikiwa na umri wa miaka 19 sasa nina umri wa miaka 46, jino limekuwa likinisumbua na kunikosesha amani ya kufanya shughuli zangu za kujitafutia kipato,” ameeleza Bi. Mdee

Bi.Mdee amesema amekuwa akifika katika hospitali hiyo kwa daktari wa meno na kumpatia ushauri kwamba aende hospitali ya Mawenzi lakini kutokana na kipato chake kuwa kidogo alishindwa kupata nauli.

“Juzi nikapata taarifa kwamba wamekuja madaktari bingwa wa Rais Samia wapo na  wa meno  leo nikasema nije ili nipate huduma na nimefika wamenipatia huduma vizuri, ni wakarimu na wamenieleza shida iliyokuwa ikinisumbua muda mrefu,” amebainisha Bi. Mdee.

Aidha,  ameshukuru kwa huduma hiyo kwasababu angekwenda Mawenzi lakini ujio wa madaktari Bingwa wa Rais Samia wamesaidia kuokoa gharama za usafiri, malazi na muda ambao angetumia kufuata huduma hizo huko Mawenzi.

 “Rais Samia ameleta madaktari bingwa katika maeneo yetu na huduma za kibingwa zinapatikana, hivyo nitoe rai kwa wananchi wenzangu kuendelea kujitokeza kwa wingi na tunamshuru sana  kwa kujali wananchi wake na kwa kuleta hawa mabingwa,” amesisitiza Bi. Mzee.

Kwa upande wake Mratibu wa Kambi ya Madaktari Bingwa wa Samia  katika mkoa wa Kilimanjaro kutoka Wizara ya Afya,  Bi.Jackline Ndanshau amewashukuru wananchi wa Same kwa kujitokeza kwa wingi na kuwataka wawe mabalozi wa hospitali hiyo kwani kwa sasa huduma za kibingwa zinapatikana hapo.

Share To:

Post A Comment: