Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amesema katika kuendelea kuimarisha Huduma za Afya hapa nchini lengo la Serikali ni kuhusisha jamii moja kwa moja kwa kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 

Prof. Nagu  amebainisha hayo  leo Oktoba 12, 2024  Jijini Arusha katika Kikao cha Kamati ya Wataalam wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii (CHTF) .                                                                        

“Kama tunataka kufanya matokeo chanya kwenye sekta ya Afya lazima kuhusisha Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ,hivyo sisi Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI mojawapo ya vitu tunavyovifanya  ni eneo la Kinga na katika kufanikisha hilo ni lazima tuhusishe jamii hasa kwa kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii”amesema.

Aidha, Prof. Nagu amesema ni muhimu kuwa nguvu za pamoja katika kuhakikisha Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii unatekelezwa ipasavyo.

“Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ili utekelezwe ipasavyo ni muhimu kuwa na nguvu za pamoja na kwa mwaka huu wa Fedha tunatarajia kuajiri Wahudumu wa Afya 28, 000”amesema.

Halikadhalika, katika Kikao hicho Mganga Mkuu wa Serikali amesisitiza umuhimu wa suala la uratibu ili kufikia  malengo, mfumo madhubuti wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, kuendelea kutimiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya  Dkt.Ntuli Kapologwe amesema                  mara baada ya kumaliza mafunzo  Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii watafikia kaya nyingi ambapo wamekuwa na mchango mkubwa kwenye afua mbalimbali za Afya ,Lishe na Ustawi wa Jamii.

“Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii  mmoja atakuwa na uwezo wa kufikia wastani wa kaya 70 hadi 100 kwa mwezi ambapo mara baada ya  mafunzo ya miezi mitatu ya         darasani na miezi mitatu kwa vitendo     na wamekuwa na mchango kwa mama wajawazito, masuala ya chanjo na mambo mengine “amesema Dkt. Kapologwe.

Kwa upande wake  Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Halmashauri  Tanzania Bara  Dkt. Samwel Marwa amesema amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii watakuwa na mchango mkubwa katika kuiunganisha Sekta ya Afya kwani wamekuwa na Mchango Mkubwa katika Ngazi ya Jamii.

Ikumbukwe kuwa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa rasmi Januari 31, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ambapo Septemba 19, 2024 Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alitangaza kuwa Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii  ni kuanzia Septemba 30,2024 ambapo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 11, 515 wameshaanza kupatiwa Mafunzo hayo na dhamira ya Serikali ni kufikia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 137, 294 katika Mikoa yote ya Tanzania katika kipindi cha miaka mitano katika kufikia dhana ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Share To:

Post A Comment: